14. Ameona najisi baada ya kumaliza kuswali

Swali 14: Airudie swalah yake mwenye kuona kwenye nguo yake najisi baada ya kutoa salamu kutoka katika swalah yake?

Jibu: Ambaye ataswali na katika mwili au nguo yake kuna najisi na asijue hilo isipokuwa baada ya kumaliza kuswali basi swalah yake ni sahihi kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanazuoni. Vivyo hivyo endapo alikuwa anajua jambo hilo hapo kabla kisha akaisahau wakati wa swalah na asikumbuke isipokuwa baada ya swalah, swalah yake ni sahihi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Allaah akasema:

“Nimekwishasema.”

Hivi ndivo imesihi Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Isitoshe yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja aliswali na katika viatu vyake kulikuwa na uchafu ambapo Jibriyl akamweleza jambo hilo. Matokeo yake akavivua na akaendelea na swalah yake na hakuianza mwanzo. Huu ni katika wepesi wa Allaah (Ta´ala) na rehema Zake kwa waja Wake.

Kuhusu ambaye ameswali hali ya kusahau hadathi basi anatakiwa kuirudia swalah yake kwa maafikiano ya wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah haikubaliwi pasi na twahara wala swadaqah inayotolewa kabla ya kugawanywa ngawira.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah haikubali swalah ya mmoja wenu anapopatwa na hadathi mpaka atawadhe.”

Kuna maafikiano juu yake.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 14
  • Imechapishwa: 15/08/2022