12. Vipi inatakiwa kumuamini Allaah (´Azza wa Jall) kwa njia ya upambanuzi?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 12: Vipi inatakiwa kumuamini Allaah (´Azza wa Jall) kwa njia ya upambanuzi?

Jibu: Tunathibitisha na kukiri kwa nyoyo na midomo yetu ya kwamba Allaah ni wajibu awepo. Ni mmoja pekee. Kila mmoja ni mwenye kumuhitajia Yeye na Yeye hamuhitajii yeyote. Amepwekeka kwa kuwa na ukamilifu, utukufu, ukubwa na ujalali wote. Ana ukamilifu wa kipindukia kiasi cha kwamba viumbe hawawezi kuzunguka kitu katika sifa Zake.

Yeye ni al-Awwaal ambaye hakuna kitu kabla Yake.

Yeye ni al-Aakhir ambaye hakuna kitu baada Yake.

Yeye ni adh-Dhwaahir ambaye hakuna kitu juu Yake.

Yeye ni al-Baatwin ambaye hafichikani na kitu.

Yeye ni al-´Aliyy na al-A´laa kwa dhati, ujuu wa hadhi na ujuu wa nguvu.

Yeye ni al-´Alim anayekijua kila kitu.

Yeye ni al-Qadiyr ambaye ni muweza juu ya kila kitu.

Yeye ni as-Samiy´ anayezisikia sauti zote pasi na kujali lugha na haja.

Yeye ni al-Baswir anayekiona kila kitu.

Yeye ni al-Hakiym anayehukumu viumbe Wake kwa hekima na kwa Shari´ah.

Yeye ni al-Hamiy anayehimidiwa kwa sifa na matendo Yake.

Yeye ni al-Majiyd aliye na enzi katika utukufu na ukubwa Wake.

Yeye ni ar-Rahmaan na ar-Rahiym ambaye huruma Yake imeenea kote na kukizunguka kila kilichopo.

Yeye ni al-Malik na al-Maalik anayekimiliki kila kitu. Mbingu na ardhi ni Vyake. Vyote hivyo ni waja Wake na wanaendeshwa na Allaah.

Yeye ni al-Hayy aliye na uhai mkamilifu uliokusanya sifa Zake zote za dhati.

Yeye ni al-Qayyuum aliye kivyake na vyengine viko kwa ajili Yake.

Ni Mwenye kusifika kwa matendo Yake yote. Anafanya kile Anachotaka. Anachotaka, huwa, na Asichotaka, hakiwi.

Tunashuhudia kuwa Yeye ndiye Mola wetu na mtengeneza sura aliyeumba viumbe kwa njia ya kihohari.

Tunashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah ambaye anastahiki kuabudiwa.

Hatunyenyekei kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Haturejei wakati wa kutubia kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Hatuelekei kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Yeye ndiye tunayemwabudu na Yeye ndiye ambaye tunamtaka msaada. Yeye ndiye ambaye tunamtarajia na kumcha.

Tunatarajia huruma Yake na tunachelea uadilifu na adhabu Yake. Hatuna Mola mwengine asiyekuwa Allaah. Tunamuuliza na kumuomba Yeye. Hatuna mungu mwengine wa kuabudu asiyekuwa Yeye. Tunamtarajia. Yeye ndiye Mola wetu anayeitengeneza dini yetu na dunia yetu. Yeye ndiye mbora kabisa wa kunusuru na kutulinda na kila chenye kudhuru na kibaya.

MAELEZO

Maneno ya mtunzi:

“Tunathibitisha na kukiri kwa nyoyo na midomo yetu… “

Bi maana tunathibitha na kutambua kunakoenda sambamba na nyoyo na midomo. Mioyo kwa kulisadikisha na kuamini jambo hilo na midomo kwa kutamka jambo hilo.

Maneno yake:

“… ya kwamba Allaah ni wajibu awepo.”

Bi maana Allaah ndiye Mungu wa haki na kwamba uwepo Wake ndio uwepo wa kikweli. Vilivyopo havina Mungu mwengine asiyekuwa Yeye.

Maneno yake:

“Ni mmoja pekee. Kila mmoja ni mwenye kumuhitajia Yeye na Yeye hamuhitajii yeyote.”

Hapa kunathibitishwa umoja Wake ambao uko ndani ya Suurah “al-Ikhlaasw”. Tunaposema kuwa ni mmoja basi makusudio ni kwamba ni mmoja katika sifa Zake. Yeye ndiye Mwenye kusifika kwa sifa kamilifu ambazo hashirikiani kwazo yeyote. Kusema kwamba kila mmoja ni mwenye kumuhitajia Yeye makusudio ni kwamba Yeye ndiye mwenye kuombwa wakati wa haja. Inaweza vilevile kuwa na maana kwamba sio mtupu tofauti na viumbe wa ardhini kama mfano wa watu na majini. Viumbe vyote vya ardhini ni watupu. Kwa msemo mwingine wanahitajia riziki ili waweze kupata uhai.

Maneno yake mtunzi:

“Amepwekeka kwa kuwa na ukamilifu, utukufu, ukubwa na ujalali wote.”

Amepwekeka kwa kila ukamilifu kwa njia ya kuachia. Tunaposema kuwa Allaah ni mjuzi tunamaanisha kuwa na elimu kamilifu kwa njia zote kabisa ambayo hapitwi na chochote katika elimu Yake. Tunaposema kuwa Allaah ni muweza tunamaanisha kuwa na uwezo mkamilifu kwa njia zote kabisa ambao hashindikana na chochote.

Maneno yake mtunzi:

“Yeye ni al-Awwaal ambaye hakuna kitu kabla Yake.”

Ni wajibu kuamini kuwa Yeye ndiye wa Kwanza, kama ambavo Yeye mwenyewe amejisifia hilo na akamsifu Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wewe ndiye wa Kwanza; ambaye hakuna kabla yako kitu. Wewe ndiye wa Mwisho; ambaye hakuna baada yako kitu. Wewe ndiye uliye Dhahiri; ambaye hakuna juu yako kitu. Wewe ndiye Umefichikana; ambaye hakuna chochote kimefichikana Nawe.”[1]

Waja hawawezi kumsifu kwa njia bora kuliko hii. Hayawahusu zaidi ya hayo. Hawawezi zaidi ya hivo. Kwa sababu hakuna yeyote anayejua chochote kuhusu sifa hii, kama alivyotuelezea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Jalla wa ´Alaa) pia ametuelezea kuhusu kubaki Kwake pindi kila kitu kitapotoweka:

كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ

“Kila kitu ni chenye kuangamia isipokuwa uso Wake.”[2]

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

“Kila aliyekuwa juu yake [ardhi] ni mwenye kutoweka na utabakia uso wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu.”[3]

Viumbe wote watatokomea isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) pindi atapozikamata mbingu kwa mkono Wake wa kuume na ardhi kwa mkono Wake wa kushoto (na mikono Yake yote miwili ni ya kuume), kisha atazitikisa na atasema:

“Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?” Kisha atazikunja ardhi saba kwenye mkono Wake wa kushoto. Kisha atasema: “Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?”[4]

Mtunzi wa kitabu amesema:

“Yeye ni al-´Aliyy na al-A´laa kwa dhati, ujuu wa hadhi na ujuu wa nguvu.”

Yeye yuko juu ya ´Arshi kwa dhati Yake. Sambamba na hilo ni Mwenye kuwadhibiti viumbe Wake wote na ni mtambuzi wa yote wanayofanya.

Sifa nyenginezo zote zimefasiriwa na mtunzi wa kitabu. Hii ndio ´Aqiydah ya Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (Rahimahu Allaah).

Yeye ni al-´Alim anayekijua kila kitu.

Yeye ni al-Qadiyr ambaye ni muweza juu ya kila kitu.

Yeye ni as-Samiy´ anayezisikia sauti zote pasi na kujali lugha na haja.

Yeye ni al-Baswir anayekiona kila kitu.

Yeye ni al-Hakiym anayehukumu viumbe Wake kwa hekima na kwa Shari´ah.

Yeye ni al-Hamiy anayehimidiwa kwa sifa na matendo Yake.

Yeye ni al-Majiyd aliye na enzi katika utukufu na ukubwa Wake.

Yeye ni ar-Rahmaan na ar-Rahiym ambaye huruma Yake imeenea kote na kukizunguka kila kilichopo.

Vivyo hivyo sifa Zake za kidhati kama mfano wa al-Qayyum ambaye ni Mwenye kujisimamia Mwenyewe na wengineo. Kila kitu ni chenye kumuhitajia na Yeye hamuhitajii yeyote. Ni Mwenye kusifika kwa sifa zote za kimatendo. Yeye ni Mwenye kufanya akitakacho. Akitakacho, huwa, na asichokitaka, hakiwi.

Maneno yake mtunzi:

“Tunashuhudia kuwa Yeye ndiye Mola wetu na mtengeneza sura aliyeumba viumbe kwa njia ya kihohari.”

Tunashuhudia ya kwamba Yeye (Subhaanah) ndiye ambaye katuumba, katuunda na katutia sura sisi na viumbe wengine wote kwa njia sanifu na ya kihodari. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ

“Ambaye amekifanya uzuri kila kitu alichokiumba.”[5]

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ

”Hakika Tumemuumba mwanaadamu katika umbile bora kabisa.”[6]

 يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ

“Ee mwanadamu! Nini kilichokughuri juu ya Mola wako mkarimu? Ambaye amekuumba akakusawazisha na akakupima na kukulinganisha sawa. Katika sura aliyotaka akakutengeneza.”[7]

Allaah ameziinua mbingu, akazipamba mbingu za dunia kwa nyota na akalifanya jua, mwezi na sayari kwenda kwa mtindo wake. Ameiumba ardhi na akawafanya majini, watu na viumbe wengine wote kuishi ndani yake. Kila kitu kimeumbwa na Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kama tulivyotaja, akakisanifu na akakipa maumbile yake kwa vile inavyonasibiana nacho.

Maneno yake mtunzi:

“Tunashuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah ambaye anastahiki kuabudiwa.”

Makusudio ni unyenyekevu wa ´ibaadah. Kuhusu unyenyekevu unaotokana na utenzwaji nguvu na khofu ya kimaumbile kwa mwengine sio ´ibaadah kama tulivyotangulia kutaja.

Maneno yake mtunzi:

“Haturejei wakati wa kutubia kwa mwengine asiyekuwa Allaah.

Haturejei wala kumwelekea mwengine asiyekuwa Allaah. Yeye ndiye Mungu wa haki.

Maneno yake mtunzi:

“Yeye ndiye tunayemwabudu na Yeye ndiye ambaye tunamtaka msaada. Yeye ndiye ambaye tunamtarajia na kumcha.

Tunatarajia huruma Yake na tunachelea uadilifu na adhabu Yake.”

Muislamu anatakiwa kuogopa uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuogopa asije kumuadhibu kwa dhambi zake. Amesema (Ta´ala):

 وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

“Hatukuwadhulumu, lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao wenyewe.”[8]

وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا

“Na watakuta yale [yote] waliyoyatenda yamehudhuria. Na Mola wako Hamdhulumu yeyote.”[9]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu.”[10]

Yeye (Subhnaanah) ni Mwenye huruma kwa waja Wake na mpole kwao, lakini huwapa baadhi ya adhabu wale wenye kumuasi. Akiwaadhibu, anafanya hivo kwa uadilifu, na akiwasamehe na akawarehemu, anafanya hivo kwa fadhilah Zake. Tunamuomba Allaah atufanye miongoni mwa wale wenye kumjua ukweli wa kumjua, kumwabudu ipasavyo na atulinde kutokamana na njama Zake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hii ndio maana mtunzi wa kitabu amesema:

“Hatuna Mola mwengine asiyekuwa Allaah. Tunamuuliza na kumuomba Yeye. Hatuna mungu mwengine wa kuabudu asiyekuwa Yeye. Tunamtarajia. Yeye ndiye Mola wetu anayeitengeneza dini yetu na dunia yetu. Yeye ndiye mbora kabisa wa kunusuru na kutulinda na kila chenye kudhuru na kibaya.”

[1] Muslim (2713).

[2] 28:88

[3] 55:26-27

[4] Muslim (2788).

[5] 32:7

[6] 95:4

[7] 82:6-8

[8] 16:118

[9] 18:49

[10] 04:40

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 66-72
  • Imechapishwa: 12/10/2021