Swali: Baadhi ya watu – Allaah atuongoze sisi na wao – wanakosa swalah ya mkusanyiko pasi na udhuru. Wengine wanatoa udhuru kwa kazi zao za kidunia na wakati mtu anawapa nasaha watu hawa wanaendelea juu ya ukaidi wao. Bali wanarudiarudia siku zote kwamba swalah ni kwa ajili ya Allaah na si haki ya yeyote kuingilia kati. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Kunasihiana kati ya waislamu na kukemea maovu ni miongoni mwa mambo ya wajibu muhimu zaidi. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote katika nyinyi mwenye kuona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa kuzungumza. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo wake. Hiyo ni imani dhaifu mno.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Dini ni kupeana nasaha.” Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwa Allaah, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wa kawaida.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Hapana shaka kwamba kuacha kuswali katika mkusanyiko ni miongoni mwa maovu ambayo ni lazima kuyakemea. Ni lazima kwa wanamme kuswali swalah tano katika misikiti kutokana na dalili nyingi. Miongoni mwazo ni kama ifuatavyo:

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”[4]

Ameipokea Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy na wengineo. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim. Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba:

“Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Ni wajibu kwa muislamu pindi anapokatazwa na ndugu yake maovu basi asikasirike na asijibu isipokuwa kheri. Badala yake anatakiwa kumshukuru na kuombea mema kwa vile amemlingania kumtii Allaah na kumkumbusha haki yake. Haijuzu kwake kufanya kiburi juu ya mlinganizi wa haki. Allaah amemsema vibaya anayefanya hivo na amemtishia adhabu ya Jahannam:

 وَإِذَا قِيلَ لَهُ اتَّقِ اللَّـهَ أَخَذَتْهُ الْعِزَّةُ بِالْإِثْمِ ۚ فَحَسْبُهُ جَهَنَّمُ ۚ وَلَبِئْسَ الْمِهَادُ

”Anapoambiwa: ”Mche Allaah”, basi hupandwa na kiburi kinachomfanya kutenda madhambi. Basi Jahannam inamtosheleza na mahali pabaya palioje pa kupumzikia!”[6]

[1] 09:71

[2] Muslim (70) na an-Nasaa´iy (4922).

[3] Muslim (82).

[4] Ibn Maajah (785).

[5] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[6] 02:206

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/29-30)
  • Imechapishwa: 12/10/2021