08. Faida ya pili baada ya kujua yaliyotangulia

Faida ya pili: Unatakiwa kuwa na khofu juu ya yale yaliyowapata watu, usije kuangamia na usije kuteleza. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ

”Hakika wale wanaomuogopa Mola wao katika hali ya ghaibu watapata msamaha na ujira mkubwa.”[1]

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”[2]

 Alipowataja watu wa Peponi alisema:

ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ

“Hayo ni kwa yule anayemkhofu Mola wake.”[3]

ذَٰلِكَ لِمَنْ خَافَ مَقَامِي وَخَافَ وَعِيدِ

”Haya ni kwa yule anayekhofu kusimamishwa mbele Yangu na akakhofu maonyo Yangu.”[4]

Wanamwogopa Allaah wasije kuteleza, wasije kutumbukia ndani ya shirki, wasije kuritadi kutoka katika dini na wasije kuipa kipaumbele dunia juu ya Aakhirah. Mtu anatakiwa kuogopa na kutahadhari. Pamoja na kwamba unatakiwa kufurahi kutokana na fadhilah na rehema za Allaah na kukuwepesishia uongofu, pia watakiwa kumcha Mola Wako. Mtu anatakiwa kuogopa moyo wake usije kupinda au kuteleza kwa sababu ya kuzembea, kufanya mchezo, kuitanguliza dunia mbele ya Aakhirah au mengineyo katika sababu za kuritadi. Hivi ndivo anavokuwa muumini. Anatakiwa kufurahi kwa sababu ya fadhilah za Allaah, amshukuru Allaah kwa kumjaalia kuwa Muislamu, anyooke barabara, apambane na nafsi yake kwa ajili ya Allaah na wakati huohuo aogope asije kutekeleza, moyo wake usije kupinda, asije kutumbukia katika yale waliyomtumbukia wengi katika kumshirikisha Allaah. Hii ndio hali ya muumini. Allaah amesema kuhusu Mitume na wafuasi Wake:

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa shauku na khofu na walikuwa wenye kutunyenyekea.”[5]

Amesema tena kuhusu mawalii Wake:

إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ

“Hakika wale ambao kwa kumuogopa Mola wao ni wenye kuogopa na wale ambao Aayah za Mola wao wanaziamini na wale ambao Mola wao hawamshirikishi na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Mola wao.”[6]

Pamoja na kuwa ni wema lakini nyoyo zao zinaogopa. Hivi ndivo wanavokuwa waumini, Mitume na wafuasi wao. Wanafanya matendo mema na wanajitahidi katika kheri. Pamoja na haya wanamwogopa Allaah, wanaogopa wasije kupinda na wanaogopa nyoyo zao zisije kupotea. Si wenye kujiaminisha. Wanaogopa na wanashika tahadhari. Hivi ndivo wanavokuwa waumini katika hali ya khofu, woga na hali ya kushika tahadhari. Hajiaminishi na vitimbi vya Allaah:

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhuluma, hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”[7]

Wana imani ya kweli. Miongoni mwa imani ni kuwa na khofu kwa Allaah, kumcha, kumtarajia, kumuadhimisha, kumtakasia Yeye nia na kuwa na msimamo katika dini Yake. Yote haya yanaingia katika imani. Hawa ndio wenye imani na wenye kuongozwa. Wamewafikishwa kwa sababu ya imani yao, ukweli wao, Ikhlaasw yao, kumwogopa kwao Allaah, kuijali dini yao na kutahadhari kutokana na sababu za shari.

[1] 67:12

[2] 03:175

[3] 98:08

[4] 14:14

[5] 21:90

[6] 23:57-60

[7] 06:82

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 23-25
  • Imechapishwa: 12/10/2021