12- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akianza swalah kwa kusema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”[1]

Tayari imeshatangulia namna alivyomuamrisha mtu yule aliyeswali makosa. Alimwambia:

“Hakuna swalah ya mtu inayotimia mpaka atawadhe vizuri na kusema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”[2]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ufunguo wa swalah ni twahara. Inaharamishwa na Takbiyr na inahalalishwa[3] na Tasliym.”[4]

Alikuwa akinyanyua sauti yake wakati wa Takbiyr mpaka inasikiwa na wale walio nyuma yake[5]. Alipokuwa mgonjwa Abu Bakr alinyanyua sauti yake ili kuwafikishia watu[6] Takbiyr yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imamu anaposema:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

nanyi semeni:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”[7]

[1] Muslim na Ibn Maajah. Hadiyth inaashiria ya kwamba hakuwa akianza swalah kwa maneno kama “nanuia kuswali… ” na mfano wake. Ni Bid´ah kabisa kwa mujibu wa wanachuoni wote. Bali walichotofautiana ni kama ni Bid´ah nzuri au mbaya. Hata hivyo kila kilichozuliwa katika ´ibaadah ni Bid´ah. Dalili ya hilo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yenye kuenea:

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Hapa hatuwezi kulizungumzia suala hili kwa kirefu.

[2] at-Twabaraaniy kwa isnadi Swahiyh.

[3] Bi maana yale matendo ambayo Allaah ameharamisha ndani ya swalah na vilevile yale matendo ambayo Allaah amehalalisha nje ya swalah. Maana ya inaharamishwa na inahalalishwa ni “vilivyoharamishwa” na “vilivyohalalishwa”. Hadiyth inathibitisha kuwa mlango wa swalah umefungwa na haufunguliwi isipokuwa kwa kutawadha. Vilevile inathibitisha kuwa mtu anaingia ndani ya makatazo yake kwa Takbiyr na mtu hatoki ila kwa Tasliym. Haya ndio maoni ya jamhuri.

[4] Abuu Daawuud, at-Tirmidhiy na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (301).

[5] Ahmad na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[6] Muslim na an-Nasaa’iy.

[7] Ahmad na al-Bayhaqiy kwa isnadi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 13/10/2016