7 – Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu akiwa amekaa kuegemea mkono wake wa kushoto ndani ya swalah na akasema: ”Hiyo ni swalah ya mayahudi.”[1]

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Usiketi namna hiyo. Hakika kikao hicho ni cha wale wanaoadhibiwa.”[2]

[1] al-Haakim na wengineo. Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.

[2] Ahmad. Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa sharti za Muslim. Nimeiongelea katika ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy”.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hadiyth hii inakataza kikao hichi na kukatolewa sababu ya makatazo kwamba ni kikao cha wale wenye kuadhibiwa. Sababu hiyo inazidi kutilia mkazo kujiepusha na mwongozo wao. al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa Masruuq ambaye amesimulia kuwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa akichukizwa kuweka mkono kiunoni mwake na akisema:

”Mayahudi wanafanya hivo.”

Amepokea tena kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Imekatazwa kuswali kwa kuweka mikono kiunoni.”

Muslim ameipokea kwa tamko lisemalo:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu kuswali kwa kuweka mikono yake kiunoni.”

Abu Daawuud ameipokea Hadiyth hii ya Ibn ´Umar kwa tamko lisemalo:

”Amekataza mtu kutegemea mikono yake wakati anapoinuka ndani ya swalah.”

Tamko hili ni dhaifu na linapingana na Hadiyth Swahiyh. Mwalimu wa Abu Daawuud ambaye ni Muhammad bin ´Abdil-Malik al-Ghazaaliy amepwekeka katika kuisimulia na kumbukumbu yake ni mbaya. Isitoshe Imaam Ahmad na wengineo wameipokea kwa njia tofauti. Nimelijadili hili kwa kina katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (967).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 175
  • Imechapishwa: 06/11/2023