Hizi ni tofauti na zile saa kubwa zinazoning´inizwa ukutani; sauti yake inafanana na sauti ya kengele za mnara. Kwa ajili hiyo muislamu hatakiwi kuingiza saa sampuli hizo katika nyumba yake, khaswa ikiwa sauti za kengele zinaambatana na nyimbo. Big Ben huko London ni mfano wa saa hizo. Kwa masikitiko makubwa saa kama hizo zimevamiwa na waislamu mpaka zikaanza kuingia ndani ya misikiti, kwa sababu ya waislamu kuwa wajinga juu ya Shari´ah yao. Mara nyingi tunamsikia imamu anasoma ndani ya swalah baadhi ya Aayah zinazotahadharisha shirki na utatu na huku saa zinalia juu ya vichwa vyao. Imamu na maamuma wake wameghafilika katika uzembe wao.

Kila wakati ambapo nilikuwa naingia msikiti uliokuwa na saa kama hiyo, basi naharibu mlio wake bila kuharibu saa yenyewe. Kwa sababu mimi ni fundi mairi wa saa – na himdi zote njema anastahiki Allaah. Nilikuwa siwezi kufanya hivo isipokuwa baada ya kutoa kalima nikielea mtazamo wa Shari´ah juu ya suala hili na nikiwakinaisha ulazima wa kuisafisha misikiti kutokana na mambo hayo. Pamoja na hayo, wakati mwingine licha ya kukinaika kwao walikuwa hawaafikiani na fikira yangu kwa hoja kwamba eti kuna Shaykh fulani na fulani ambao wameswali katika msikiti huo pasi na kusema kitu. Haya yametokea Syria.

Sikuwahi kufikiri kuwa saa kama hizi zinazokumbushia shirki zinaweza kuingia Saudi Arabia, nchi ya Tawhiyd, mpaka mimi na ndugu yangu wa damu Muniyr tulipoingia msikiti wa Qubaa´ katika msimu wa hajj mwaka wa 1382. Tukashangazwa pindi tuliposikia sauti ya kengele ya mnara kutoka katika saa yake. Basi tukazungumza na baadhi ya wasimamizi wa msikiti na kuwakinaisha kutofaa kutumia saa kama hizi msikitini. Wakakinaika haraka sana. Lakini tulipowaomba kuharibu kengele yake, wakakataa. Wakasema kuwa sio katika jukumu lao na kwamba watalipeleka suala hilo kwa watawala. Tukasema kuwa kuna tofauti kubwa kati ya leo na jana. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kweli pale aliposema:

”Hakuna mwaka isipokuwa wa baada yake ni wenye shari zaidi mpaka pale mtapokutana na Mola wenu.”[1]

[1] Tazama “as-Swahiyhah” (1218).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 169-170
  • Imechapishwa: 01/11/2023