110. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu kuyatembelea makaburi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kwamba lau ningekuwa na uwezo juu ya Ka´bah basi ningechukua mfereji wake na ningeiwekea mifereji miwili ya mbao. Jengine kwamba eti mimi naharamisha kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isitoshe kwamba eti nakemea kutembelea makaburi ya wazazi wake wawili na wengineo. Aidha kwamba namkufurisha wenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah.

MAELEZO

Huu ni uongo juu ya Shaykh. Eti amesema:

“Kwamba lau ningekuwa na uwezo juu ya Ka´bah… “

Kwa sababu mfereji wa Ka´bah imejengwa kwa dhahabu. Wanasema kuwa Shaykh amesema:

“Kwamba lau ningekuwa na uwezo juu ya Ka´bah basi ningechukua mfereji wake na ningeiwekea mfereji wa mbao.”

Huku ni kumsemea uongo Shaykh. Hakuna ubaya kuiwekea Ka´bah mfereji wa dhahabu. Kwa sababu dhahabu haiharibiki na wala haigeuki. Ingelikuwa ya mbao ingeliwa na ardhi na ingebadilika. Shaykh hajasema kitu kabisa juu ya mfereji wa Ka´bah. Lakini walimtuhumu juu ya hili. Mpaka wakafikia kumtuhumu kuwa eti amesema kuwa bakora yake ni bora kuliko ya Mtume. Kwa sababu Mtume Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwishakufa na hamnufaishi yeyote. Lakini kwamba fimbo yake ananufaika nayo na kwamba anapiga kwayo. Huu ni uongo mkubwa kumsemea Shaykh.

Kadhalika wamedai kuwa Shaykh ameharamisha kutembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo si sahihi. Bali yeye (Rahimahu Allaah) alikuwa akitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kaburi la Mtume linatembelewa kama yanavyotembelewa makaburi mengine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[1]

Linaingia pia kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambalo linatakiwa kutembelewa na kutolewa salamu, kama yanavyotolewa salamu makaburi mengine na kutembelewa. Hakupinga matembezi yanayokubalika katika Shari´ah. Anachopinga ni matembezi ya kizushi na ya kishirki juu ya kaburi la Mtume na mengineyo. Yule ambaye anayatembelea makaburi kwa ajili ya kuwaomba wafu, anawataka msaada waliyomo ndani ya makaburi, anatafuta baraka kwao na kwa udongo wake, haya ndio ambayo wanachuoni wanapinga. Ni mamoja Shaykh na wengineo. Lakini matembezi yanayokubalika Kishari´ah ambayo mtu amekusudia salamu, kumuombea du´aa na kuzingatia hali za makaburi hakuna mwanachuoni yeyote aliyepinga hayo.

Shaykh anapinga matembezi ya makaburi ya kishirki na ya kizushi na si kwamba anapinga matembezi yaliyowekwa katika Shari´ah. Lakini wao wanawatatiza watu kwa maneno haya.

[1] Muslim (976) amepokea mfano wake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 153-154
  • Imechapishwa: 19/06/2021