Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewagawanya viumbe Wake katika mafungu matatu:

1 – Wale walioneemshwa. Ni wale ambao Allaah amewatunuku elimu na wakaitendea kazi.

2 – Wale walioghadhibikiwa. Ni wale ambao wanajua na hawatendei kazi.

3 – Wale waliopotea. Ni wale ambao wanatendea kazi pasi na elimu.

Ndio maana katika kila swalah tunamuomba Allaah atuongoze njia ilionyooka:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha… “

Nao ni wale waumini wenye kufanyia kazi yale wanayoyajua:

غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ

“… si ya walioghadhibikiwa… “

Bi maana wale wanaojua pasi na kufanya matendo. Matokeo yake wakawa wenye kukosea:

وَلَا الضَّالِّينَ

“… wala waliopotea.”

Bi maana usituongoze katika njia ya waliopotea ambao wamo ujingani na ndani ya upotofu.

Mtu anahitaji du´aa hii zaidi kuliko anavyohitaji chakula, kinywaji na kupumua. Kwa sababu mtu akikosa chakula, kinywaji na kupumua kiwiliwili chake kinakufa. Kifo ni kitu hakiepukiki, ima chaja mapema au baadaye. Kifo cha mwili hakimdhuru mtu muda wa kuwa amenyooka katika kumtii Allaah na moyo wake ukawa salama na hai. Lakini moyo wake unapokufa kwa kukosa uongofu basi unakufa moyo na roho yake na hatimaye anaingia Motoni.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 24
  • Imechapishwa: 01/02/2023