Kutubu kwa dhambi na kuendeleza nyingine

Wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wametofautiana kama tawbah ya mtu inakubaliwa pamoja na kwamba wakati huohuo kuendelea na dhambi nyingine. Kuna maoni matatu ya wanachuoni kuhusu hili:

1- Kuna ambao wanasema ni sahihi kutubu kwa dhambi ilihali mtu yuwaendelea na dhambi nyingine. Tawbah yake inakubalika kwa dhambi hii na anabaki kuwa ni mwenye kupata madhambi kwa hiyo dhambi nyingine anayofanya kwa hali yoyote ile.

2- Kuna ambao wamesema kuwa kutubu hakukubaliwi ikiwa mtu ni mwenye kuendelea na dhambi nyingine.

3- Kuna waliofafanua na kusema ya kwamba ikiwa dhambi hiyo anayoiendeleza ni katika jinsia ya dhambi ambayo ametubu juu yake, basi haikubaliwi. Na ikiwa sivyo, inakubaliwa. Mfano wa hili mtu ametubu kwa kula ribaa lakini – Allaah atukinge – anakunywa pombe na ni mwenye kuendeleza kufanya hivo. Katika hali hii kuna wanachuoni ambao wamesema kule kutubu kwake kwa kula ribaa hakukubaliki. Vipi atakuwa ni mwenye kutubia kwa Allaah ilihali anaendelea kumuasi? Wanachuoni wengine wakasema kuwa tawbah yake inakubaliwa. Kula kwake ribaa ni kitu na kunywa pombe ni kitu kingine, na haya ndio maoni ya mtunzi wa kitabu – Imaam an-Nawawiy – (Rahimahu Allaah) ya kwamba kutubu kwa dhambi kunakubaliwa pamoja na wakati huohuo kuendelea na dhambi nyingine kwa mujibu wa Ahl-ul-Haqq.

Ama ikiwa dhambi ni ya jinsia ileile, kwa mfano – Allaah atukinge – mtu amepewa mtihani wa kufanya uzinzi na amepewa mtihani mwingine wa kuwaangalia wanawake, kuwatazama kwa matamanio na mfano wa hayo. Je, kutubu kwake kwa kufanya uzinifu kunakubaliwa ilihali ni mwenye kuendelea kuwaangalia wanawake kwa matamanio au kinyume chake? Hapa pia kuna makinzano, kuko wanaosema kuwa tawbah yake inasihi na wanaosema kuwa haisihi.

Maoni sahihi juu ya masuala haya ni kwamba kutubu kwake na dhambi kunasihi pamoja na kuendelea na dhambi nyingine. Lakini hata hivyo hapewi jina la mtubiaji kwa njia ya moja kwa moja na wala hastahiki sifa walizopewa watubiaji. Hakutubia tawbah kamilifu. Tawbah yake ni pungufu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/92-93)
  • Imechapishwa: 01/02/2023