10. Elimu ni yenye kutangulia kabla ya kuzungumza na kutenda

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango unaozungumzia elimu kabla ya kauli na kitendo. “

MAELEZO

al-Bukhaariy ni Imaam Abu ´Abdillaah Muhamamd bin Ismaa´iyl ambaye alikufa mwaka wa 256 baada ya kuhajiri. Mtunzi wa “as-Swahiyh”. Ni imamu miongoni mwa maimamu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Muhaddith anayejulikana[1]. Kwa mujibu wa wakaguzi na wanazuoni wengi na Muhaddithuun kitabu chake “Swahiyh-ul-Bukhaariy” ndio kitabu sahihi zaidi baada ya Qur-aan. Baadhi ya wanazuoni wametanguliza “as-Swahiyh” ya Muslim. Lakini wale waliofanya hivo ni kwa njia ya uundwaji na mpangilio. Vinginevyo “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy ndio kitabu sahihi zaidi. Isitoshe Muslim ni mwanafunzi wa al-Bukhaariy.

Elimu ni yenye kutangulia kabla ya maneno na kutenda. Mosi mtu anatakiwa kujifunza kisha baadaye ndio azungumze na kutenda. Elimu ndio kiongozi wa hayo mawili. Mtu anapotenda pasi na elimu matendo yake yanakuwa gizani na yeye pia anakuwa ndani ya upotofu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amegawanya watu ndani ya Suurah “al-Faatihah”, ambayo ndio mama wa Qur-aan, katika mafungu matatu. Amesema (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Mfalme wa siku ya malipo.”[2]

Halafu akabainisha kuwa ndiye anastahiki kuabudiwa:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”

Kisha baada yake kukaja du´aa. Du´aa hii ni tukufu. Du´aa ambayo ni tukufu, iliyokusanya, bora na yenye manufaa zaidi ni:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.”[3]

[1] Tazama wasifu wake katika ”Siyar A´laam-in-Nubalaa” (12/391),  ”Tahdhiyb-ul-Kamaal” (09/47), “Taariykh-ul-Baghdaad” (02/322) na “Haad-us-Saariy” utangulizi wa Fath-ul-Baariy” (01/479).

[2] 01:01-04

[3] 01:06-07

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 23
  • Imechapishwa: 01/02/2023