6- Ni haramu kwa mume wake kufanya jimaa na mke pindi yuko na hedhi kama ambavyo vilevile ni haramu kwa mke kumwacha akafanya naye jimaa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake [wanapokuwa] katika hedhi. Wala msiwakaribie [kujimai nao] mpaka watwaharike.” (02:222)

Makusudio ya “hedhi” ni ile damu ya hedhi na pahali pake ambako ni ukeni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kila kitu isipokuwa jimaa.”[1]

Waislamu wamekubaliana juu ya uharamu wa kumjamii mwanamke kwenye tupu yake wakati yuko na hedhi. Si halali kwa mtu anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho kufanya dhambi hii iliyoharamishwa kwa mujibu a Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Mwenye kufanya hivo anamuasi Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kufuata njia isiyokuwa ya waumini. an-Nawawiy amesema:

“ash-Shaafi´iy amesema: “Mwenye kufanya hivo amefanya dhambi kubwa.” Wenzetu na wengine wamesema yule mwenye kuhalalisha kufanya jimaa na mwanamke mwenye hedhi ni kafiri.”[2]

Hata hivyo Allaah ameruhusu vingine vyenye kuzima matamanio ikiwa ni pamoja na busu, kukumbatia na kucheza mbali na kuepuka uke. Pamoja na hivyo lililo salama zaidi ni kutokukutana naye bila ya kizuizi baina ya kitovu na magoti. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiniamrisha kujifunga leso ambapo nafanya hivo. Baada ya hapo anacheza na mimi ilihali niko na hedhi.”[3]

[1] Muslim (302).

[2] al-Majmuu´ (2/374).

[3] al-Bukhaariy (300) na Muslim (293).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016