Miongoni mwa hekima na siri za funga ni imsaidie mja kumtii Allaah na hivyo ajitahidi kufanya mambo ya kheri na kujiepusha na mambo ya haramu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote asiyeacha maneno ya uwongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[1]

Miongoni mwa hekima za funga ni afya katika miili. Imepokelewa:

“Fungeni mtapata afya.”[2]

Miongoni mwa hekima za funga ni tajiri aweze kukumbuka matumbo ya mafukara na masikini yanayohisi njaa. Baadhi ya Salaf walipoulizwa kuhusu hekima ya kufunga wakasema:

“Ili tajiri aweze kuhisi ladha ya njaa ili asimsahau fakiri.”

Allaah ameiweka Shari´ah ya kufunga kwa ajili ya manufaa ya waislamu. Ameiweka ili kuilea miili, mazoezi ya subira na kustahamili maumivu. Ameiweka ili kuzitengeneza tabia, kuzisafisha nafsi, kuzipa adabu ya kuacha matamanio na kujiepusha na mambo yaliyokatazwa. Mfungaji anayaacha yale matamanio yake anayoyapenda kwa ajili ya kumridhisha mpendwa Wake Muumbaji (Subhaanah). Swawm ni neema kubwa inayofanya madhambi kusamehewa na kupandisha daraja. Swawm inamfanya mja kumshinda shaytwaan kwa kuzifanya nyembamba njia za chakula na kinywaji. Kutokana na matamanio shaytwaan hutembea ndani ya mishipa ya mwanadamu kama damu inavyotembea. Kwa hivyo mishipa hiyo inadhoofika kwa sababu ya swawm. Swawm inafanya mafungamano ya mja na Mola wake kuwa na nguvu zaidi kwa sababu ni kitendo kilichojificha. Kila ambavyo kitendo ni chenye kujificha zaidi ndio kinakuwa karibu zaidi na ikhlaasw.

Kwa kifupi ni kwamba funga imewekwa katika Shari´ah kwa ajili ya kumwabudu Allaah, kunyenyekea amri Yake, kumuadhimisha, kutekeleza wajibu, kujiepusha na mambo ya haramu, kulinda viungo kutokana na makosa, kuyalinda macho kutokana na kutazama ya haramu na mdomo kutokana na machafu, uwongo, matusi, usengenyi, umbea na maneno ya uwongo. Aidha kuyahifadhi masikio kusikiliza yaliyo ya haramu, kuilinda mikono kutokana na kuiba, uporaji, ghushi, maudhi na mashambulizi. Vilevile kuihifadhi miguu kuyaendea yale aliyoharamisha Allaah. Pia kuuhifadhi moyo kutokana na vifundo, chuki, hasadi na imani mbovu. Kuhifadhi utupu kutokana na yale aliyoharamisha Allaah. Mkusanyiko wa yote hayo ni: kumcha Allaah na kumchunga katika hali ya siri na dhahiri. Kama alivosema Mola wetu (Subhaanah):

لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“… mpate kuwa na taqwa.”[3]

Maana yake ni kwamba mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mumche Allaah. Himdi na shukurani zote njema anastahiki Allaah kwa neema Zake ambazo hazihesabiki wala kudhibitiwa. Sifa zote njema anastahiki Allaah ambaye kwa neema Zake yanatimia mambo mazuri.

Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] al-Bukhaariy (1903).

[2] at-Twabaraaniy (8312). al-Haythamiy amesema:

“Wapokezi wake ni waaminifu.” (Majma´-uz-Zawaaid)

[3] 02:183

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 32
  • Imechapishwa: 17/04/2023