Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Allaah ameifanya swawm kuwa na manufaa ya kilimwengu na ya kidini zaidi ya vile anavyofikiria mwanadamu. Ameipangia (Ta´ala) thawabu na malipo makubwa kiasi cha kwamba endapo nafsi iliyofunga ingeyawaza, basi ingeruka kwa furaha na ingelitamani mwaka mzima uwe Ramadhaan ili daima aendelee kuburudika.

Allaah ameweka Shari´ah ya kufunga ili muislamu aweze kujipamba kwa uchaji Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa.”[1]

Allaah (Ta´ala) ameweka Shari´ah ya swawm ili iwe njia kubwa ya kuweza kumcha (Subhaanah). Kumcha Allaah kumekusanya kheri zote za duniani na Aakhirah. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُوا اللَّـهَ

”Hakika Tumewausia wale waliopewa Kitabu kabla yenu na nanyi [pia tunakuusieni] kwamba: “Mcheni Allaah.”[2]

Kumcha Allaah ndio sababu ya kuondolewa matatizo, hakuna jambo muhimu zaidi kwa mja kama Allaah kumtosheleza katika mambo ya dini na dunia yake na ni sababu ya mja kutunukiwa riziki ya halali kwa njia asiyokuwa anaitarajia. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ

“Na yule anayemcha Allaah, basi humjaalia njia [ya kutokea] na atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii.”[3]

Anayemtegemea Allaah amemcha Allaah na mfungaji ni miongoni mwa wenye kumcha Allaah. Isitoshe yuko chini ya utoshelevu wa Allaah. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ

”Ee Nabii! Anakutoshele za Allaah na anayekufuata miongoni wa waumini.”[4]

Kumcha Allaah ni sababu ya mja kuwepesishiwa mambo yake. Amesema (Subhaanah):

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا

“Na yeyote yule anayemcha Allaah, basi atamjaalia wepesi katika jambo lake.”[5]

Kumcha Allaah ni sababu ya kusamehewa makosa na kulipwa malipo makubwa. Amesema (Subhaanah):

ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُعْظِمْ لَهُ أَجْرًا

”Hiyo ni amri ya Allaah amekuteremshieni. Na yeyote anayemcha Allaah, basi atamfutia maovu yake na atamuadhimishia malipo.”[6]

Anayemcha Allaah basi Allaah hutia moyoni mwake nuru ambayo inamfanya kuweza kupambanua kati ya haki na batili na kufutiwa makosa na madhambi yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ

”Enyi walioamini! Mkimcha Allaah atakupeni Upambanuzi na atakufutieni maovu yenu na atakusamehe; na Allaah ni Mwenye fadhilah kubwa.”[7]

[1] 02:183

[2] 04:131

[3] 65:02-03

[4] 08:64

[5] 65:04

[6] 65:05

[7] 08:29

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 31
  • Imechapishwa: 11/05/2023