Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hakika swawm ina fadhilah kubwa na nyingi ikiwa ni pamoja na zifuatazo:

1 – Funga ni kinga na inamlinda mfungaji kutokana na madhambi na Moto pia. Imepokelewa katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni kinga. Itapokuwa ni siku ya funga ya mmoja wenu, basi asizungumze maneno machafu wala asipige kelele. Mtu akimtukana au akamgombeza, basi amwambie: “Mimi nimefunga. Mimi nimefunga.”[1]

2 – Allaah ameiegemeza swawm Kwake kati ya matendo mengine yote. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amesema: “Matendo yote ya mwanadamu ni yake, isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu na mimi ndiye Nitailipa.”[2]

3 – Harufu ya mdomo imtokayo mfungaji ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Kama ilivyo katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ile harufu imtokayo mdomoni mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”[3]

4 – Swawm na vivyo hivyo swalah na swadaqah ni kafara ya mtu kupewa mtihani juu ya familia yake, mali yake na jirani yake katika yale maneno yasiyostahiki katika magomvi, maneno, ghadhabu au matusi yanayomtokea kwa familia au jirani yake. Vilevile yale yanayomtokea wakati anapojishughulisha na mali. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Tulikuwa tumekaa kwa ´Umar tahamaki akasema: “Ni nani kati yenu ambaye amehifadhi maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu fitina?” Nikasema: “Mimi kama alivosema.”Akasema: “Hakika wewe juu yake yeye au juu yake [fitina hiyo] ni mwenye ujasiri.” Nikasema: “Mtihani wa mtu juu ya famili yake, mali yake, mtoto wake au jirani yake inasamehewa kwa ajili ya swalah, swawm, swadaqah na kuamrisha na kukataza.”[4]

5 – Ambaye anafunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio anasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayesimama usiku wa Qadr hali ya kuwa na imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Yule atakayefunga Ramadhaan hali ya kuwa na imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[5]

Kusamehewa kumefungamanishwa na sharti hii; hali ya kuwa na na imani na matarajio. Kwa maana nyingine mtu amwamini Allaah, Mtume Wake, asadikishe Shari´ah Yake na atarajie ujira na thawabu. Kwa msemo mwingine afunge hali ya kumtakasia nia Allaah pekee na si kwa kujionyesha, kufuata kibubusa na isionekane amefunga ili asende kinyume na watu. Aidha kunaongezwa sharti nyingine ambayo ni lazima ili mtu aweze kusamehewa madhambi: kutekeleza mambo ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ilioko kwa Muslim:

“Swalah tano, ijumaa moja mpaka nyingine na Ramadhaan mpaka Ramadhaan nyingine ni vyenye kufuta yaliyo kati yake midhali mtu atajiepusha na madhambi makubwa.”[6]

Vilevile Allaah amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Mkijiepusha madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.”[7]

6 – Peponi kuna mlango kwa ajili ya wafungaji unaoitwa “ar-Rayyaan” ambao wataingia ni wao tu pasi na wengine. Hilo limethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Sahl (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Peponi upo mlango unaoitwa ar-Rayyaan. Wataingia kupitia mlango huo wafungaji siku ya Qiyaamah na si wengine. Kutasemwa: ”Wako wapi wafungaji?” Wasimame na hawatoingia wengine zaidi yao. Wakishaingia utafungwa na hakuna yeyote mwingine atakayeingia.”[8]

7 – Mfungaji atakapokutana na Mola wake atafurahia funga yake. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfungaji ana furaha mbili; furaha ya kwanza wakati anapofungua na furaha nyingine wakati atapokutana na Mola wake. Harufu ya mdomo imtokayo mfungaji ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski.”

Furaha ya mfungaji kwa kukutana na Mola wake ni kutokana na yale malipo na thawabu atazoziona. Atatimiza malipo aliyopangiwa kwa kukubaliwa swawm yake ambayo Allaah amemjaalia.

Kuhusu furaha ya mfungaji wakati wa kufungua sababu yake ni kukamilika kwa ´ibaadah yake, kusalimika kwake kutokana na vifunguzi vyake na zile thawabu zake anazozitaraji kwa vile imetimia swawm yake, kumalizika kwa ´ibaadah yake na kuruhusiwa kula, jambo ambalo linaendana na maumbile yake na hivyo inaondoka njaa na kiu chake.

Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151).

[2] al-Bukhaariy (7492) na Muslim (1151).

[3] al-Bukhaariy (7492) na Muslim (1151).

[4] al-Bukhaariy (525) na Muslim (144).

[5] Muslim (1901) na Muslim (760).

[6] Muslim (233).

[7] 04:31

[8] al-Bukhaariy (1896) na Muslim (1152).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 17/04/2023