08. Hatua na awamu ilizopitia funga ya Ramadhaan

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hekima ya Mjuzi wa yote na Mwenye khabari za ndani na za nje ilipelekea uwekwaji Shari´ah wa kufunga Ramadhaan upitie hatua na awamu mbalimbali kutokana na hekima Yake Allaah na rehema inayonasibiana na hali za waja:

1 – Mara ya kwanza mja alikuwa akipewa chaguo kati ya kufunga na kula kisha baadaye amlishe chakula masikini kwa kila siku iliyompita, ingawa kufunga ndio ilikuwa bora. Hapo ni pale aliposema (Ta´ala):

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]!”[1]

Baada ya Allaah kusema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Kufunga swawm kwenyewe ni] siku za idadi maalum. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo. Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]! Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[2]

2 – Swawm ikawajibishwa kwa mkazi, mzima, muweza na ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia. Lakini ukifika wakati wa kufungua na jua likazama kisha mtu akalala kabla ya kufungua au akaswali ´Ishaa, basi papohapo chakula kinakuwa haramu kwake, kinywaji na tendo la ndoa mpaka usiku unaofuatia. Wakapata uzito na ugumu mkubwa.

3 – Kukafanywa halali kula, kunywa na tendo la ndoa usiku wa swawm kuanzia wakati wa kuzama kwa jua mpaka wakati wa kuchomoza kwa alfajiri. Allaah (Ta´ala) akateremsha juu ya hilo:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu; wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkizihini nafsi zenu hivyo akapokea tawbah yenu na akakusameheni. Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[3]

al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)) walipokuwa wakifunga kisha ikatokea kuwa walale bila ya kufuturu, walikuwa wakiendelea kufunga usiku na mchana mpaka ifike jioni tena [ya siku ya pili]. Siku moja Qays bin Swirmah Answaariy alikuwa amefunga. Ulipofika wakati wa kufungua, alimwendea mkewe na kumuuliza: “Je, una chakula?” Akajibu: “Hapana, lakini hebu nende kukutafutia.” Na [Qays siku hiyo] alikuwa akifanya kazi ngumu ukamshinda usingizi. Mkewe akaja [akiwa na chakula] wakati alimpokuta amelala alisema: “Khasara ni kwako!” Ilipofika katikati ya mchana wa siku ya pili, alizimia. Yakatajwa hayo kwa Mtume na hapo ndipo ikatremka Aayah ifuatayo:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu… “

Wakafurahi juu yake furaha kubwa. Pia kukateremka:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi Kisha timizeni funga mpaka usiku.”[4] [5]

Katika Hadiyth hii kula na vifunguzi vyengine kumefungamanishwa na kulala. Pia kumefungamanishwa makatazo ya hayo katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwa swalah ya ´Atamah ambayo ni ´Ishaa. Ameipokea Abu Daawuud kwa tamko lisemalo:

“Watu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakishaswali ´Atamah, basi chakula, kinywaji na jimaa inakuwa ni haramu kwao na wanafunga mpaka siku inayofuatia.”[6]

Salamah bin Akwaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Wakati kuliposhuka Aayah hii:

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

“Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini.”[7]

ikawa anayetaka anafunga na anayetaka anakula na baada ya hapo anawalisha chakula masikini.” Hali iliendelea hivo mpaka kulipoteremshwa Aayah hii:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”[8][9]

Ameipokea Muslim.

Kupitia maandiko haya imebainika kuwa jambo Shari´ah imethibiti juu yake kuhusu swawm ya Ramadhaan ni ulazima wa kufunga kwa ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia, mzima, mkazi kihakika. Haijuzu kwake kula mchana wa Ramadhaan. Allaah amemruhusu mfungaji kula wakati wa usiku kuanzia pale jua linapozama mpaka kuchomoza kwa alfajiri. Himdi zote njema anastahiki Allaah kwa yale aliyowepesisha, akasahilisha, akaneemesha, akafanya upole na thawabu kubwa kwa waja Wake waumini. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu.

Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 02:184

[2] 02:183-184

[3] 02:187

[4] 02:187

[5] al-Bukhaariy (1915).

[6] Abu Daawuud (2313).

[7] 02:184

[8] 02:184

[9] Muslim (1145)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 17/04/2023