07. Dalili za kufaradhishwa swawm ya Ramadhaan

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hakika kufunga Ramadhaan ni faradhi miongoni mwa faradhi za Uislamu kubwa na ni moja miongoni mwa nguzo za Uislamu. Msingi wa hilo ni Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Dalili juu ya hilo ni dhahiri na ziko wazi na kutambulika kwa waislamu wa kawaida, sembuse wasomi.

Kufunga Ramadhaan kulifaradhishwa katika mwaka wa pili baada ya kuhajiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafunga Ramadhaan tisa kwa maafikiano.

Allaah amewafaradhishia ummah kufunga mwezi mmoja kila mwaka; nao ni mwezi wa Ramadhaan. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Kufunga swawm kwenyewe ni] siku za idadi maalum. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo. Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]! Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Fungeni siku mlizowekewa] ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na mpate kushukuru.”[1]

Vilevile imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim ambao wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji na kufunga Ramadhaan.”[2]

Katika Hadiyth hii tukufu kuna ya kwamba Uislamu umejengeka juu ya nguzo tano na kwamba kufunga Ramadhaan ndio msingi na nguzo ya tano katika nguzo za Uislamu ambao Uislamu umejengeka juu yake.

Imethibiti pia kwa al-Bukhaariy na Muslim ambao wamesimulia:

“Bedui mmoja alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kichwa chake kikiwa timtim akasema: “Nieleza ni kipi ambacho Allaah amefaradhisha juu yangu katika swalah?” Akasema: “Swalah tano; isipokuwa kama utapenda kujitolea kitu.” Akasema: “Nieleza ni kipi ambacho Allaah amefaradhisha juu yangu katika swawm?” Akasema: “Kufunga Ramadhaan; isipokuwa kama utapenda kujitolea kitu.” Akasema: “Nieleza ni kipi ambacho Allaah amefaradhisha juu yangu katika zakaah?” Akasema: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamweleza Shari´ah za Uislamu. Bedui yule akasema: “Naapa kwa Yule ambaye amekukirimu; sintojitolea chochote na wala sintopunguza chochote katika yale ambayo Allaah amefaradhisha juu yangu.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Amefaulu akiwa mkweli” au “ataingia Peponi akiwa mkweli.”[3]

Katika Hadiyth hii kuna dalili inayoonyesha kuwa ambaye atafanya mambo ya wajibu na mambo ya faradhi na wakati huohuo akaacha mambo ya haramu, basi amefaulu na kwamba ni katika watu wa Peponi kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Amefaulu akiwa mkweli” au “ataingia Peponi akiwa mkweli.”

Baada ya bedui yule akasema:

”… sintopunguza chochote katika yale ambayo Allaah amefaradhisha juu yangu.”

Hawa ndio watu wa kati na kati na wema. Wakiongezea juu yake yale mambo yanayopendeza na mambo ya kujitolea – katika swalah, swawm, swadaqah, hajj, jihaad na mengineyo – basi wanakuwa ni miongoni mwa wale waliotangulia na waliokurubishwa, ambao ndio wako na ngazi za juu. Wakifanya upungufu katika baadhi ya mambo ya wajibu, wakayaacha baadhi yake au wakafanya baadhi ya mambo ya haramu, basi wanakuwa wamejidhulumu nafsi zao. Nao pia ni katika watu wa Peponi ijapo kabla ya hapo wanaweza kufikwa na matatizo, hali za kutisha na adhabu ndani ya kaburi. Watu sampuli hii tatu ndio walioteuliwa na watu wa Peponi ambao Allaah amewarithisha Kitabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ

“Kisha Tukawarithisha Kitabu wale tuliowateuwa miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni aliyedhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa kati na kati na miongoni mwao aliyetangulia kwa mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah – hiyo ndio fadhilah kubwa.”[4]

Tunamuomba Allaah Mkarimu katika fadhilah Zake.

Miongoni mwa dalili za kufaradhishwa kufunga Ramadhaan ni pamoja na yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga ´Aashuuraa´ na akawaamrisha watu kuifunga. Wakati ilipofaradhishwa Ramadhaan ikaachwa.”[5]

Maana ya kwamba funga ya ´Aashuuraa´ iliachwa ni kwa njia ya ulazima na ikabakia hali ya kupendeza.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kuwa Quraysh walikuwa wakifunga ´Aashuuraa´ katika kipindi kabla ya kuja Uislamu. Baadaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha kuifunga mpaka ilipofaradhishwa Ramadhaan ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mwenye kutaka aifunge na mwenye kutaka ale.”[6]

Miongoni mwa dalili zinazoonyesha kuwa kufunga Ramadhaan ni faradhi ni Hadiyth ya Jibriyl inayotambulika ambayo ameipokea Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwa kifupi ambapo Jibriyl anamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu nini Uislamu, imani, ihsaan na lini Saa. Wakati alipomuuliza kuhusu Uislamu basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijibu kwa kusema:

“Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ukiweza kuiendea… ”

Yeyote atakayepinga kufaradhishwa na ulazima wa kufunga ni kafiri na mwenye kuritadi nje ya Uislamu. Kwa sababu amepinga faradhi na nguzo kuu miongoni mwa nguzo za Uislamu na pia jambo linalotambulika vyema katika Uislamu. Atakayekubali ulazima wa kufunga Ramadhaan na akala kwa makusudi pasi na udhuru, basi ametenda dhambi kubwa inayomfanya kuwa fasiki. Lakini hakufurishwi kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Licha ya hivyo atalazimishwa kufunga. Mtawala wa Kishari´ah atamlazimisha kufunga kwa kumfunga jela au kumpiga bakora au yote mawili. Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa akila Ramadhaan bila udhuru anakufuru. Tunamuomba Allaah usalama kutokana na kila baya na pia tunamuomba uthabiti juu ya dini mpaka wakati wa kufa.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake zote.

[1] 02:183-185

[2] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[3] al-Bukhaariy (1891) na Muslim (11).

[4] 32:35

[5] al-Bukhaariy (1892).

[6] al-Bukhaariy (1893) na Muslim (1125).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 21-24
  • Imechapishwa: 17/04/2023