Kama alivosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah):

”Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipochukia baragumu ya mayahudi inayopulizwa kwa mdomo na kengele za mnara za manaswara zinazopigwa kwa mkono, akatoa sababu ya machukizo yake kwamba ni katika matendo ya mayahudi na manaswara. Majulisho ya hukumu hulengwa sababu ya hukumu hiyo. Haya yanafahamisha makatazo juu ya yale mambo ambayo ni ya mayahudi na manaswara. Haya licha ya kwamba pembe ya mayahudi ina msingi kwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyekuwa akipuliza kwenye baragumu. Kuhusu kengele ya mnara ya manaswara ni jambo limezuliwa. Kwa sababu mambo mengi ya Shari´ah ya manaswara yamezuliwa na marabi na watawa   wao. Haya yanajulisha kuwa sauti zote hizo zimechukizwa kwa hali yoyote ile, ni mamoja zinahusiana na swalah au kitu kingine, kwa sababu ni katika mambo ya mayahudi na manaswara. Manaswara hupiga kwenye kengele za minara yao katika nyakati mbalimbali na si nyakati za ´ibaadah peke yake. Nembo ya dini safi na pwekeshi ni adhaana ambayo ndani yake kuna kutangaza utajo wa Allaah ambayo kwayo hufunguliwa milango ya mbingu, mashaytwaan wakakimbia na ikashuka rehema.

Wafalme wengi wa ummah huu wamepewa majaribio ya nembo hizi za mayahudi na manaswara. Alkhamisi hii niliwaona wakifukiza moshi na wakipiga kengele ndogo. Bali wako baadhi ya wafalme ambao wakipiga tarumbeta na kupiga midundo unapofika wakati wa zile swalah tano. Haya ndio yaleyale ambayo yalimchukiza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam). Wengine walikuwa wakipiga midundo mara mbili mchana kwa ajili ya madai yao ya kumwigiliza Dhul-Qarnayn. Yako mengine yaliyofanywa na wafalme wa pembeni.

Wakati wafalme wa Mashariki na mfano wao walipoanza kujifananisha na mayahudi, manaswara na wasiokuwa waarabu katika warumi na wafursi na wakaicha njia ya waislamu, ndipo wakaingia katika yale yanayomchukiza Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo Allaah akawafanya makafiri wa kituruki wawashinde – vita ambavyo viliahidiwa – na kuwaweka wananchi na miji katika hali ambayo nchi za Kiislamu hazijawahi kuona mfano wake. Hayo yanathibitisha maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shubiri kwa shubiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”[1]

Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na hata baada yake, waislamu walikuwa wanatambulika wakati wa vita kuwa na utulivu na kumtaja Allaah. Qays bin ´Abbaad, ambaye ni mmoja katika wanafunzi wakubwa wa Maswahabah, amesema:

”Walikuwa wanapendeza kushusha sauti chini wakati wa Dhikr, vita na mazishi.”

Mapokezi mengine vilevile yanaashiria kuwa walikuwa watulivu katika mazingira haya na wakati huohuo nyoyo zao zimejaa kumtaja na kumtukuza Allaah (´Azza wa Jall). Hali zao zilikuwa vivyo hivyo wakati wa swalah. Jambo la kupandisha sauti katika sehemeu hizi tatu ilikuwa ni miongoni mwa mambo ya watu wa Kitabu na wasiokuwa waarabu. Baadaye jambo hilo wakatahiniwa nalo wengi katika ummah huu.”[2]

[1] al-Bukhaariy (4356) na Muslim (2669).

[2] Iqtidhwaa’-us-Swiraat al-Mustaqiym, uk. 56

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 167-168
  • Imechapishwa: 01/11/2023