108. Ndio maana huandikwa matendo ya watu

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna chochote katika hayo kinachopotea ujuzi wa Mola wao. Malaika wa kifo huchukua roho kwa idhini ya Mola wake.

MAELEZO

Kuandikwa kwa matendo ya waja haina maana kwamba Allaah hayajui – bali Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anayajua. Hata hivyo yanaandikwa ili yaweze kumkabili mja siku ya Qiyaamah. Kila mmoja atajionea mwenyewe matendo na kukisoma kitabu chake mwenyewe. Allaah haadhibu kutokana na ujuzi anaoujua juu ya mja, bali anaadhibu kutokana na kitendo cha mja. Pindi kitendo kinapofanywa basi Malaika hukiandika na kukilinda ndani ya kitabu. Kitabu hichohicho ndicho atakachopewa mja siku ya Qiyaamah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا

“Kila mtu Tumemfungia matendo yake shingoni mwake na tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu akutane nacho hali ya kuwa kimekunjuliwa. [Ataambiwa]: “Soma kitabu chako nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabu.””[1]

Ikiwa mja alikuwa miongoni mwa watu wazuri basi atapokea daftari lake kwa mkono wa kuume. Akiwa alikuwa miongoni mwa watu waovu basi atapokea daftari lake kwa mkono wa kushoto. Atayaona matendo yake na hatokanusha chochote. Vinginevyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anajua kila kitu, lakini hata hivyo hamwadhibu mtu kutokana na elimu Yake iliotangulia ya kujua yale yatakayofanywa na watu mpaka wayafanye. Kwa ajili hiyo anawaadhibu kutokana na matendo yao au huwakirimu kutokana na matendo yao.

[1] 17:13-14

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 81
  • Imechapishwa: 01/09/2021