107. Radd juu ya uongo wa Ibn Suwhaym kwamba Shaykh tofauti za wanachuoni ni adhabu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Eti mimi nasema kuwa kutofautiana kwa wanachuoni ni adhabu.

MAELEZO

Huku ni kumsemea uongo Shaykh. Kwa sababu kutofautiana kwa wanachuoni katika mambo ya matawi na mambo ya Ijtihaad sio adhabu. Wanachuoni wamejitahidi na wakatafiti. Wakipatia wanapata thawabu mara mbili na wakikosea wanapata thawabu mara moja. Ijtihaad ni jambo linalotakikana na kutofautiana ndani yake mtu hasemwi vibaya. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakijitahidi katika fatwa ambapo kila mmoja anasema kwa vile ambavyo dalili imemdhihirikia. Hii ni aina fulani ya tofauti yenye kusemwa vizuri. Kwa sababu ni kuitafuta haki.

Tofauti yenye kusemwa vibaya ni ile tofauti katika haki. Haijuzu kutofautiana katika haki baada ya kuwa imekwishabainika. Bali ni lazima kuitendea kazi haki na wala haijuzu kwenda kinyume nayo.

Kwa hiyo tofauti imegawanyika aina mbili:

1- Tofauti yenye kusemwa vibaya. Amesema (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[1]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakatofautiana baada ya kuwajia hoja za wazi.”[2]

Kufarikiana na kutofautiana ni jambo linalosemwa vibaya. Kitu chenye kusababisha kuendelea juu ya haki na kushabikia batili ni chenye kusemwa vibaya.

2- Tofauti ambayo mtu anatafuta ndani yake haki. Tofauti hii ni yenye kusemwa vizuri. Mwenye kupatia anapata thawabu mara mbili na mwenye kukosea anapata thawabu mara moja. Tukishajua kuwa amekosea sisi hatuchukui maoni yake bali tunachukua maoni ya yule aliyepatia. Hili ndio jambo linalotakikana. Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni wakasema:

“Hakuna kukemeana katika mambo ya Ijtihaad.”

Kwa mfano Tahiyyat-ul-Masjid wakati ambao imekatazwa kuswali ndani yake. Baadhi ya wanachuoni wanaona kuwa mtu aswali vivyo hivyo kwa kutendea kazi maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atapoingia mmoja wenu msikitini basi asiketi chini mpaka kwanza aswali Rak´ah mbili.”[3]

Wamesema kuwa amri hiyo ni yenye kuenea. Ni mamoja wakati uliokatazwa na wakati mwingine. Kwa sababu ni katika mambo yenye sababu. Pamoja na kwamba jopo la wanachuoni wengi wanaona kuwa haifai kuswali wakati uliokatazwa. Si Tahiyyat-ul-Masjid wala Nawaafil nyenginezo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuswali baada ya ´Aswr mpaka jua lizame. Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuswali baada ya Fajr mpaka jua lichomoze[4]. Kwa hiyo wakatanguliza ueneaji wa makatazo mbele ya ueneaji wa amri. Kwa hiyo yule mwenye kutendea kazi maoni haya hakaripiwi na yule mwenye kutendea kazi yale maoni ya kwanza hakaripiwi. Kwani kina mmoja kuna anapotegemea. Jengine ni kwamba haya ni mambo ya Ijtihaad ambayo haijuzu kuvuka mpaka ndani yake. Maswahabah walikuwa wakitofautiana katika mambo ya mataga na udugu wao unaendelea.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliporudi kutoka katika vita na akawaandaa Maswahabah kwa ajili ya kwenda kupambana vita na mayahudi wa Banuu Quraydhwah akasema:

“Asiswali mmoja wenu ´Aswr isipokuwa Banuu Quraydhwah.”

Baadhi ya Maswahabah wakasema kuwa malengo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuharakisha na si kwamba anakusudia kuwa tusiswali isipokuwa mpaka tufike Banuu Quraydhwah. Matokeo yake wakaswali walipokuwa njiani. Baadhi ya wengine wakasema kuwa Mtume amesema:

 “Asiswali mmoja wenu ´Aswr isipokuwa Banuu Quraydhwah.”[5]

Kwa hiyo wakachelewesha ´Aswr mpaka walipofika Banuu Quraydhwah. Walipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukemea upande wowote. Kwa sababu kila mmoja katika wao ametendea kazi dalili. Ijtihaad ya aina kama hii hakuna kukemeana ndani yake. Haisemwi kuwa ni dhabu. Bali inatakiwa isemwe kuwa ni Ijtihaad na kuitafuta haki.

[1] 03:103

[2] 03:105

[3] al-Bukhaariy (444) na Muslim (714) kupitia kwa Abu Qataadah as-Salamiy (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] al-Bukhaariy (588) na Muslim (825) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[5] al-Bukhaariy (946, 4119) na Muslim (1770) na tamko ni lake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 147-149
  • Imechapishwa: 07/06/2021