105. Radd juu ya uongo wa Ibn Suwhaym kwamba Shaykh anabatilisha madhehebu manne

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah anajua zaidi kuwa bwana huyo amenisemea uongo mambo ambayo sikuyasema na mengi katika hayo hayakunijia hata akilini mwangu. Kwa mfano amesema:

Mimi navibatilisha vitabu vya madhehebu manne na kwamba eti mimi nasema kuwa watu tokea miaka mia sita hawako juu ya lolote.

MAELEZO

Je, ni kweli kwamba Shaykh anabatilisha vitabu vya madhehebu manne? Huu ni uongo mkubwa kabisa. Shaykh amesoma juu ya madhehebu ya Hanaabilah. Hafuati kibubusa madhehebu ya Hanaabilah. Bali anachukua yale yaliyosimama juu ya dalili kutoka katika madhehebu ya ash-Shaafi´iy, madhehebu ya Maalik au madhehebu ya Abu Haniyfah. Huu ndio mfumo wa Shaykh. Yeye katika msingi anafuata madhehebu ya Imaam Ahmad. Lakini wakati wa kujibu anafuata yaliyo na nguvu kwa mujibu wa dalili. Ni mamoja yanatokana na madhehebu ya Imaam Ahmad au ya mwengineo. Hafuati kichwa mchunga. Bali ni mwenye kukusudia haki. Huu ndio mfumo wake katika fatwa na kufunza. Anachukua yale yenye dalili zenye nguvu kutoka katika madhehebu yoyote miongoni mwa yale madhehebu manne. Lakini hatoki nje ya madhehebu manne. Maneno ya Ibn Suwhaym huyu juu ya Shaykh:

“Anabatilisha vitabu vya madhehebu manne.”

Huu ni uongo. Kwa sababu yeye (Rahimahu Allaah) hakutoka nje ya madhehebu manne. Bali yeye anafaidika nayo na anajibu kwa mujibu wa yale yenye dalili zenye nguvu katika hayo. Ni mamoja yameafikiana na madhehebu yake ya Hanbaliy au hayakuafikiana nayo. Kwa sababu ni mwenye kukusudia haki.

Maneno yake:

“Kwamba watu tokea miaka mia sita hawako juu ya lolote.”

Kwa msemo mwingine yeye anawakufurisha watu. Huu ni moja ya uongo wa Ibn Suwhaym kwamba Shaykh anawakufurisha watu. Kwa nini anawakufurisha watu? Kwa sababu analingania katika Tawhiyd na kukemea shirki. Kwa kufanya hivo ndio wanadai kuwa anawakufurisha watu. Hakuna jengine analofanya zaidi ya kuwalingania watu katika Tawhiyd na kukemea shirki. Hakukufurisha watu. Hakumkufurisha isipokuwa yule ambaye kumethibiti ukafiri wake kwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, kama ilivyotajwa katika vile vichunguzi kumi alivyondika.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 146
  • Imechapishwa: 03/06/2021