Swali: Wako baadhi ya vijana wana ufahamu wa kimakosa kuelewa ni nani mwanachuoni. Hilo limepelekea mtu ambaye si mwanachuoni, anayeipa nyongo dunia, mfanya ´ibaadah au mtoa mawaidha, anafanywa na yeye ni katika wanazuoni. Matokeo yake wamefanywa kuwa marejeo katika masomo, maelekezo, mafundisho na mengineyo. Tunapendelea utueleze mwanachuoni ni mtu gani.

Jibu: Ibn-ul-Qayyim amemweleza mwanachuoni kwa njia yenye kuenea pale aliposema:

”Elimu ni kutambua uongofu kwa dalili yake. Hilo haliwezi kulinganishwa na kufuata kichwa mchunga.”

Hii ndio elimu. Mwanachuoni ni yule mwenye kuitambua haki kwa dalili. Huyu ndiye mwanachuoni.

Elimu inaweza kuwa yenye kubobea kwa njia ya kwamba mtu ana elimu juu ya mambo mengi. Kitu hichi ndio huitwa ”uwezo katika mambo ya hukumu”.

Pia mtu anaweza kuwa mwanachuoni katika suala moja. Anaweza kwa mfano akachukua vitabu vya wanazuoni na akatafiti mada fulani, akazidurusu dalili za wanazuoni na akawa ni mwanachuoni katika mada hiyo peke yake. Kwa mnasaba wa jambo hilo imepokelewa Hadiyth:

”Fikisheni kutoka kwangu ijapokuwa Aayah moja.”

Watoa mawaidha wengi hutaja dalili zisizokuwa na msingi na dhaifu na malengo yao wanachotaka ni kuwatia watu nguvu kufanya mambo yanayotakikana na kuwatahadharisha kutokamana na mambo yanayotakiwa kuepukwa. Wanachukulia wepesi katika mlango wa kuvutia na kuogopesha. Hapana shaka yoyote kwamba watu hawa wananufaisha, lakini hawatakiwi kuchukuliwa kama marejeo katika elimu ya Shari´ah kwa njia ya kwamba mtu akategemea maneno yao isipokuwa pale watakaposema maneno yaliyojengeka juu ya maneno ya Allaah na Hadiyth Swahiyh za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule atakayekuja na elimu iliyo na dalili itakubaliwa.

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) alitahadharisha wanazuoni wasiokuwa na uelewa. Uelewa maana yake ni kwamba mtu awe na hekima kwa njia ya kwamba mtu analiweka kila jambo mahala pake na awe na dalili itakuwa ni hoja yake mbele ya Allaah (´Azza wa Jall).

Vinginevyo nadhani kwamba watu wengi wanapambanua kati ya mwanachuoni na mwanafunzi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (64 B)
  • Imechapishwa: 03/06/2021