Hivyo ikabainika kutokana na Aayah zilizotangulia kwamba kuacha uongofu wa makafiri na kujifananisha nao katika matendo, maneno na matamanio yao ni miongoni mwa makusudio na malengo ambayo yamewekewa msingi na Qur-aan na baadaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akayabainisha na kuwapambanulia nayo ummah katika mambo mengi ya Shari´ah. Mayahudi waliliona hilo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakahisi kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anachotaka ni kwenda kinyume nao katika mambo yao yanayowahusu wao peke yao. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Pindi wake wa mayahudi walipokuwa wanapata hedhi basi wanawafukuza majumbani na hawali, hawanywi wala kuchanganyika nao majumbani. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya hilo ndipo kukateremshwa:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi.”

Kwa hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Changanyikeni nao na fanyeni kila kitu isipokuwa tu tendo la ndoa”. Hayo yakawafikia mayahudi wakasema: ”Bwana huyu anachotaka ni yeye kujitofautisha nasi katika kila kitu.” Usayd bin Hudhwayr na ´Abbaad bin Bishr wakaja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Mayahudi wanasema kadhaa na kadhaa. Je, tusiwajamii wakati wako na hedhi?” Uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ukabadilika mpaka tukafikiria kuwa ametukasirikia.” Wakatoka nje na wakakutana na bwana mmoja aliyekuja na maziwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwagiza kwao na kuwapa maziwa wanywe. Ndipo wakatambua kuwa hakuwakasirikia.”[1]

[1] Muslim, Abu ´Awaanah na Abu Daawuud (2165) na tamko ni lake. at-Tirmidhiy amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 165-166
  • Imechapishwa: 30/10/2023