103. Mfano wa wapinzani wa Shaykh na tuhuma zao mbalimbali za uongo dhidi yake

Maneno yake:

“Jengine ni kwamba nyote mnatambua kuwa nimefikiwa na khabari kwamba barua ya Sulaymaan bin Suwhaym imewafikieni.”

Pindi alipobainisha ´Aqiydah yake akataka kumraddi ambaye amemtuhumu kwa tuhuma ambazo yeye yuko mbali nazo. Tuhuma kama hizi hasalimiki nazo si Mtume wala wafuasi wa Mitume. Wote hutuhumiwa pindi wanapolingania kwa Allaah na kukemea yale yanayofanywa na watu wa batili. Huwaelekezea tuhuma mbalimbali kwamba wanatafuta utawala, ufalme, mali, kutaka kuonekana na kusikika, kwamba ni wachawi, kwamba ni wendawazimu na tuhuma nyenginezo mbalimbali. Hayo yametajwa ndani ya Qur-aan maneno mbalimbali ya makafiri wanapowatuhumu Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na khaswakhaswa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walimtuhumu kwamba ni mshairi, kwamba ni mwendawazimu, kwamba ni mfundishwaji, kwamba ni mwongo na kwamba anatafuta uongozi juu ya watu – tusemeje wanachuoni walio chini yake kama mfano wa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab?

Wakati alipolingania ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walimtuhumu, wakamsemea na kumzulia uongo. Uongo wao umeandikwa na kujibiwa katika vitabu mbalimbali vilivyowekwa ndani ya “ad-Durar-us-Suniyyah fiyl-Ajwibah an-Najdiyyah”. Ndani yake kuna vitabu vya kujitegemea kama mfano wa “Miswbaah-udh-Dhwalaam fiy man kadhaba ´alaash-Shaykh al-Imaam wat-Tahamahu bitakfiyr ´alaa Ahl-il-Islaam” cha Shaykh ´Abdul-Latwiyf bin ´Abdir-Rahmaan (Rahimahu Allaah). Pia kuna Radd dhidi ya Daawuud Jarjiys al-´Iraaqiy kutokana na ile batili aliyoandika. Pia kuna Radd dhidi ya Dahlaan kwenye kitabu kwa jina Swiyaanatu al-Insaan ´alaa waswasat-is-Shaykh Dahlaan”. Dahlaan huyu alikuwa ni Muftiy wa watu wa Makkah. Alikuwa ni khurafi ambaye alikuja na shubuha mbalimbali dhidi ya Da´wah ya Shaykh ambapo akaanza kumsemea uongo na akaandika kitabu akakipa jina “ad-Durar as-Saniyyah fiyr-Radd ´alaa al-Wahhaabiyyah”. Ndani yake alitaja uzushi juu ya Shaykh ambapo akaraddiwa na mwanachuoni mmoja miongoni mwa wanachuoni wa India ambaye ni Muhammad Bashiyr as-Sahsawaaniy (Rahimahu Allaah) kwa kitabu alichokipa jina “Swiyaanatu al-Insaan ´alaa waswasat-is-Shaykh Dahlaan.” Ni kitabu kilichochapishwa na kipo. Mfano wa kitabu kingine ni “Ghaayatu al-Amaaniy fiyr-Radd ´alaa an-Nabhaaniy” cha Shaykh Hamuud Shukriy al-Aalusiy.

Miongoni mwa uzushi wa Dahlaan ni kwamba anasema kuwa eti Ibn ´Abdil-Wahhaab alikuwa akidhamiria akitaka kudai utume. Lakini alipoona kuwa watu hawatomsadikisha ndio akanyamazia fikira hii. Vinginevyo ni kitu kilikuwa moyoni mwake[1]. Ni kama kwamba Dahlaan huyu anajua yaliyomo ndani ya moyo na anajua mambo yaliyofichikana. Kuna uongo na uzushi mwingine wa kuchekesha. Kwa hiyo Shaykh si yeye peke yake ambaye alituhumiwa na akawekewa shubuha katika Da´wah yake. Ikiwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walituhumiwa basi wafuasi wao wana haki zaidi ya kufanyiwa hivo. Amesema (Ta´ala) kumwambia Mtume Wake:

مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ

“Hakusemwi juu yako isipokuwa kile walichoambiwa Mitume kabla yako. Hakika Mola wako ni Mwenye msamaha na Mwenye adhabu iumizayo.”[2]

[1] Tazama ”Swiyaanatu al-Insaan ´alaa waswasat-is-Shaykh Dahlaan”, uk. 512.

[2] 41:43

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 142-144
  • Imechapishwa: 03/06/2021