101. Namna Khawaarij na Mu´tazilah wanavyoamrisha mema na kukataza maovu

Maneno yake Shaykh:

“… kwa mujibu wa vile inavopelekea Shari´ah.”

Hii ni Radd ya maneno ya Khawaarij na Mu´tazilah kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu ni kule kuwafanyia uasi watawala, kuleta mpasuko, kufarikisha umoja na kumwaga damu kwa hoja ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Haya si kwa mujibu wa Shari´ah. Bali ni jambo linalokatazwa na Shari´ah. Wala kufanya hivi sio kuamrisha mema na kukataza maovu. Wao wanaita jambo la kujivua katika utiifu wa watawala, kuleta mpasuko, kuhalalisha damu za waislamu na kuwakufurisha, wanaita mambo haya kwamba ni kuamrisha mema na kukataza maovu. Huu ni upindaji katika jina hili tukufu. Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh-ul-Islaam, na wengineo katika Ahl-us-Sunnah, amesema:

“… kwa mujibu wa vile inavopelekea Shari´ah.”

Hayo yamesemwa pia na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah katika “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”[1]. Yote hayo ni ili watu wasije kuitakidi juu ya jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu yale waliyoitakidi Khawaarij na Mu´tazilah ambao wanamzingatia kuwa ni kafiri yule muumini mwenye kufanya dhambi kubwa na wanaita jambo hilo kwamba ni katika kukataza maovu, jambo ambalo ni kinyume na vile inavopelekea Shari´ah. Isitoshe ni kuchupa mpaka katika kuamrisha mema na kukataza maovu.

Kwa hivyo ni wajibu kuzinduka juu ya jambo hili na kwamba vile inavopelekea Shari´ah ni kama alivosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo  wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”

Hii ndio namna ya kuamrisha mema na kukataza maovu kwa kiasi cha uwezo wa mtu. Asipoweza mtu basi hakulazimishwa jambo hilo. Isipokuwa tu ni lazima ukataze kwa moyo wako na uwatenge watu wake na ujiweke nao mbali.

Kuhusu wale ambao wanabeba silaha dhidi ya nyuso za waislamu na wanasema kuwa huko ndio kuamrisha mema na kukataza maovu, haya ni madhehebu ya Khawaarij na madhehebu ya Mu´tazilah wapotevu.

Hiki ndio kidhibiti walichokusudia wanachuoni pale waliposema:

“… kwa mujibu wa vile inavopelekea Shari´ah.”

[1] Uk. 47.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 140-141
  • Imechapishwa: 02/06/2021