100. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya kuamrisha mema na kukataza maovu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naona uwajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu kwa mujibu wa vile inavopelekea Shari´ah safi ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Shaykh, kama wengineo katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, anaona ulazima wa kuamrisha mema na kukataza maovu. Amesema (Ta´ala):

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚوَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Wawepo kutoka kwenu watu wanaolingania kheri na kuamrisha mema na unaokataza maovu. Hao ndio waliofaulu.”[1]

 كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora uliotolewa kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[2]

Zipo Aayah nyenginezo.

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[3]

Amefanya katika sifa zao ni kwamba wanaamrisha mema na wanakataza maovu. Ambaye haamrishi mema na hakatazi maovu ni miongoni mwa wanafiki. Amesema (Ta´ala):

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ

“Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake wenyewe kwa wenyewe: wanaamrisha maovu na wanakataza mema.”[4]

Wao wako kinyume. Hivi sasa hapa wanaamrisha maovu. Bali wanaamrisha maovu kwa aina zake zote, wanalingania kwayo, wanawalingania waislamu kuiacha dini yao, wanaita kushikamana barabara na dini kwamba ni msimamo mkali na uchupaji mpaka. Wanasema kwamba ni lazima waislamu waachane na jambo hilo. Wanasema kwamba ni lazima kwa wanawake wafanye uasi wa kindoa na waachane na Hijaab, kwamba watu waache kuwapenda waumini peke yake na kuwachukia makafiri na kwamba wawafanye watu wote kuwa sawasawa na wasiwatofautishe. Huku ni kuamrisha maovu. Wao wanaamrisha maovu na wanakataza maovu siku zote na daima. Kinyume cha waumini ambao wanaamrisha mema na kukataza maovu.

Kuamrishana mema na kukatazana maovu ni miongoni mwa mambo ya lazima ya dini. Ni jambo ambalo ni la lazima katika Uislamu. Kukipatikana jambo la kuamrishana mema na kukatazana maovu basi hiyo ni alama ya kufaulu kwa Ummah. Kukikosekana jambo la kuamrishana mema na kukatazana maovu basi hiyo ni alama ya kuangamia kwa Ummah. Amesema (Ta´ala):

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّنْ أَنجَيْنَا مِنْهُم

“Basi kwanini hawakuweko katika karne za kabla yenu, watu weledi wanakataza ufisadi katika ardhi isipokuwa wachache kati ya Tuliowaokoa miongoni mwao!”[5]

Wachache ndio waliokuwa wakiamrisha mema na kukataza maovu na ndipo Allaah akawaokoa kutokamana na adhabu:

فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ أَنجَيْنَا الَّذِينَ يَنْهَوْنَ عَنِ السُّوءِ وَأَخَذْنَا الَّذِينَ ظَلَمُوا بِعَذَابٍ بَئِيسٍ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ

“Waliposahau yale waliyokumbushwa nayo, basi Tuliwaokoa wale wanaokemea maovu na tukawapatiliza wale waliodhulumu kwa adhabu mbaya kabisa kwa yale waliyokuwa wakifanya ufasiki.”[6]

Hawasalimiki isipokuwa wale wenye kuamrishana mema na kukatazana maovu. Kuhusu yule ambaye haamrishi mema na kukataza maovu basi huyo ima ni mnafiki ambaye ndani ya moyo wake hakuna imani au ni muumini mwenye imani dhaifu. Wanapoangamia waovu basi huangamia pamoja nao. Kwa sababu hakuamrisha mema na kukataza maovu kwa kiasi cha uwezo wake. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فإن لم يستطع فبلسانه، فإن لم يستطع فبقلبه، وذلك أضعف الإيمان

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Nyuma ya hilo hakuna imani sawa na mbegu ya hardali.”[7]

Ni dalili iliyofahamisha kwamba ambaye haamrishi mema na kukataza maovu ni mwenye kuangamia pamoja na wenye kuangamia. Kwa hiyo ni lazima kuamrisha mema na kukataza maovu. Hakupatikani suala la kuokoka isipokuwa kwa kuwepo jambo hili. Kukikosekana jambo la kuamrishana mema na kukatazana maovu watu wanastahiki kuangamia.

[1] 03:104

[2] 03:110

[3] 09:71

[4] 09:67

[5] 11:116

[6] 07:165

[7] Muslim (50) kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 139-140
  • Imechapishwa: 02/06/2021