10. Makatazo ya kuchunguza Qadar


Elimu nyenginezo zote zilizozuka baada ya zama za Maswahabah na zikazingatiwa kuwa ni elimu na wale watu wake katika mazingira ya kwamba yule ambaye hakuzijua wakamchukulia kuwa ni mjinga au mpotofu, si chochote isipokuwa ni katika mambo yaliyozuliwa yaliyokatazwa. Mfano wa elimu hizo ni yale yaliyozua Mu´tazilah juu ya Qadar na wakampigia mifano Allaah. Isitoshe kumepokelewa makatazo ya kupekua Qadar. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hali ya Ummah huu itaendelea kuwa yenye kunyooka muda wa kuwa hawazungumzii juu ya watoto na Qadar.”[1]

Ameipokea Ibn Hibbaan na al-Haakim. Imepokelewa kama maneno kutoka kwa Swahabah, kitu ambacho baadhi yao wamekitilia nguvu.

al-Bayhaqiy amepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakitajwa Maswahabah zangu basi nyamazeni. Zikitajwa nyota basi nyamazeni.”

Imepokelewa kupitia njia nyingi na katika cheni za wapokezi wake kuna walakini.

Imepokelewa kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alisema kumwambia Maymuun bin Mihraan:

“Tahadhari kutazama kwenye nyota, kwa sababu kunapelekea katika ukuhani. Tahadhari na Qadar, kwa sababu kunapelekea katika uzandiki. Tahadhari kumtukana yeyote katika Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Allaah akakutupa ndani ya Moto juu ya uso wako.”

Abu Nu´aym amepokea upokezi ulioko juu kama maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kitu ambacho hakikusihi.

Kupekua Qadar kumekatazwa kutokana na sababu zifuatazo:

1 – Mtu anagonganisha Aayah za Allaah baadhi kuzigonga zengine ambapo yule mwenye kuthibitisha na mwenye kukanusha wanaingia katika mizozo. Kitu kama hichi kilitokea kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akaghadhibika na kukataza jambo hilo. Mambo kama hayo ni katika jumla ya zile tofauti na mizozo juu ya Qur-aan, kitu ambacho kimekatazwa.

2 – Mtu ima akathibitisha au pia akakanusha Qadar kwa kutumia akili. Mfano wa kipimo cha akili ni maneno ya Qadariyyah:

“Allaah atakuwa dhalimu akiadhibu kwa kitu ambacho tayari amekwishapanga na kukikadiria.”

Au maneno ya wale waliokwenda kinyume nao:

“Allaah amewatenza nguvu waja juu ya matendo yao.”

3 – Mtu anapekua siri ya Qadar, kitu ambacho kimekatazwa na ´Aliy na wengine katika Salaf. Kwani hakika viumbe kamwe hawawezi kufikia ujuzi wa uhakika wa Qadar.

[1]Ibn Hibbaan (1824) na al-Haakim (1/33) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 50-54
  • Imechapishwa: 15/09/2021