Mfano wa mambo ya uzushi ni yale yaliyozuliwa na Mu´tazilah na vifaranga vyao wanapozungumza kuhusu dhati na sifa za Allaah (Ta´ala) kwa dalili za kiakili. Ni jambo la khatari zaidi kuliko kuzungumzia Qadar kwani kuzungumza juu ya Qadar ni kuzungumza juu ya matendo Yake ilihali huku ni kuzungumza juu ya dhati na sifa Zake.

Watu hawa wamegawanyika katika mafungu mawili:

1 – Anayepinga mengi katika yale yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Hoja yao ni kuwa eti wanaona kuwa ni kumfananisha na sifa za viumbe. Kwa mfano Mu´tazilah wanasema:

“Lau Angelionekana, basi angelikuwa kiwiliwili. Kwa sababu hakuonekani isipokuwa katika upande fulani.”

Vilevile wanasema:

“Lau Angelizungumza maneno yanayosikika basi Angelikuwa kiwiliwili.”

Wameungwa mkono na wale wanaokanusha kulingana. Wakaikanusha kwa sababu wanaona eti kunapelekea kufananisha. Huu ni mwenendo wa Mu´tazilah na Jahmiyyah.

Salaf wameafikiana juu ya kwamba watu hawa walikuwa wazushi na wapotofu. Wengi katika wale watu waliokuja nyuma wanaojinasibisha na Sunnah na Hadiyth wamechukua mengi katika mapito ya watu hawa.

2 – Ambaye anathibitisha yote hayo kwa kutumia akili isiyokuwa na msingi. Maoni yao yameraddiwa. Mfumo huo alikuwa nao pia Muqaatil bin Sulaymaan na wafuasi wake kama Nuuh bin Abiy Maryam na baadhi ya Muhaddithuun, hapo kale na baadaye. Mapito hayo wako nayo Karraamiyyah. Baadhi yao wamezithibitishia sifa hizi kiwiliwili, ima kimatamshi au kimaana. Wengine wamemthibitishia Allaah sifa ambazo hazikutajwa na Qur-aan wala Sunnah, kama kutikisika. Salaf wamekaripia i´tiqaad ya Muqaatil wakati alipomraddi Jahm kwa kutumia dalili ya akili. Walimponda kwa ususuwavu na wako miongoni mwao ambao walifikia hata kuhalalisha kuuawa. Miongoni mwao ni Makkiy bin Ibraahiym, mwalimu wa al-Bukhaariy na wengine.

Mfumo sahihi ni ule waliochukua Salaf katika kuzipitisha Aayah na Hadiyth za sifa kama zilivyokuja pasi na kuzifasiri, kuzifanyia namna, kuzilinganisha, kuingia kwa undani katika maana au kipimo. Haikusihi kutoka kwa mmoja yeyote katika wao, na khaswakhaswa Imaam Ahmad, kwamba alionelea kinyume.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 15/09/2021