Kadhalika usomaji wa kina katika elimu ya nasaba ni kitu kisichohitajika. Imekwishatangulia kwamba ´Umar na wengineo wamelikataza, licha ya kuwa Maswahabah na jopo la wanafunzi wa Maswahabah kadhaa walikuwa wanaijua na wanaitilia bidii.

Vivyo hivyo kubobea katika elimu ya kiarabu na sarufi. Ni kitu kinachomshughulisha mtu na zile elimu ambazo ni muhimu zaidi. Kujishughulisha na mambo kama hayo kunamkosesha mtu elimu yenye manufaa. Kwa ajili hiyo al-Qaasim bin Mukhaymirah amechukizwa na elimu ya sarufi na akasema:

“Mwanzo wake ni ushughulishaji na mwisho wake ni upetukaji.”

Anakusudia kuingia sana kwa ndani katika mada hiyo. Kwa ajili hiyo Ahmad amechukizwa kubobea katika lugha na maneno geni. Alifikia hata kumkaripia Abu ´Ubayd juu ya jambo hilo na akasema:

“Ni kitu kinachomshughulisha mtu na yale ambayo ni muhimu zaidi.”

Ndio maana ilikuwa inasemwa kwamba kiarabu katika mazungumzo ni kama chumvi ndani ya chakula; mtu atumie kile kiasi kitachomtosheleza katika kuyatengeneza maneno, kama ambavo inatumika chumvi kiasi tu kinachofanya chakula kuonjeka vizuri. Kiwango  kikubwa chenye kuzidi kitaharibu tu.

Pia elimu ya hesabu inahitajika katika kutambua mirathi, wasia na zile mali zinazogawanywa kwa wale wenye kuzistahiki. Mengine yote yenye kuzidi ni katika mambo yasiyohitajika zaidi tu ya kuipa akili chemshabongo isiyokuwa na haja ambayo inamshughulisha na ambayo ni muhimu zaidi.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 15/09/2021