10. Je, inafaa kupangusa juu ya kila kinachofunika mguu?

Swali 10: Baadhi ya wanazuoni wanaona kufaa kupangusa juu ya kila chenye kufunika mguu. Je, ni sahihi?

Jibu: Maoni haya ndio sahihi. Dalili zinazojuzisha kufuta juu ya soksi za ngozi zimekuja kwa njia ya kuachia. Hazikufungamanishwa kwa sharti zozote. Yale ambayo Shari´ah imeyataja kwa njia ya kuachia basi haitofaa kuyafungamanisha kwa sharti zozote. Kufanya hivo ni kubana yale ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameyatanua. Kimsingi ni kwamba yale yaliyotajwa kwa kuachia yanabaki kama yalivyoachiwa na yaliyotajwa kwa jumla yanabaki kwa ujumla wake mpaka kuwepo dalili inayofungamanisha au kukifanya kuwa maalum. Baadhi ya Shaafi´iyyah wamenukuu kwamba ´Umar na ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wamejuzisha kufuta juu ya soksi zilizo nyembamba. Haya yanasapoti yale maoni yanayosema kufaa kupangusa juu ya soksi nyembamba na zilizo na matundu.

Maoni sahihi pia ni kwamba inafaa kupangusa juu ya bendeji. Bali kupangusa juu ya bendeji kunatakiwa kufaa zaidi kutokana na ule uzito wa kuivua na kuivaa tena. Haya yanaafikiana na maneno ya Allaah (Ta´ala) pale alipotaja Aayah ya twahara, kuoga na Tayammum:

مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Allaah hataki kukufanyieni magumu wowote, lakini anataka kukusafisheni na akutimizieni neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.”[1]

[1] 05:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/166-167)
  • Imechapishwa: 05/05/2021