09. Ni lazima soksi ziwe zimesalimika na matundu?

Swali 09: Baadhi ya wanazuoni wameshurutisha kwamba soksi na soksi za ngozi zinatakiwa kufunika ile sehemu yote ya mguu ambayo inalazimika kuoshwa ili ifae kupangusa juu yake. Je, ni sahihi?

Jibu: Sharti hii si sahihi kwa kuwa haina dalili yoyote. Maadamu chenye kufunika mguu kinaitwa “soksi ya ngozi” au “soksi” basi itakuwa inajuzu kupangusa juu yake. Sunnah imejuzisha kupangusa juu ya soksi ya ngozi kwa njia isiyofungamana. Yale ambayo Shari´ah imeyataja kwa njia isiyofungamana basi haitakiwi kwa yeyote kuyafungamanisha isipokuwa kwa kupatikana dalili kutoka katika Qur-aan, Sunnah, maafikiano au kipimo sahihi.

Kujengea juu ya hili inajuzu kupangusa kwenye soksi za ngozi zilizopasukapasuka na soksi za ngozi nyembamba. Wengi katika Maswahabah walikuwa ni mafukara. Mafukara wengi soksi zao za ngozi hazisalimiki kuwa na matundu. Ikiwa hali mara nyingi ni kama hivi au ilukuweko kwa wingi katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  kuzindua jambo hilo, basi inafahamisha kwamba sio sharti. Lengo la soksi za ngozi sio kulinda ile ngozi; lengo la soksi za ngozi ni kuufanya ule mguu uhisi joto na ziunufaishe. Sababu iliyopelekea kujuzu kupangusa juu ya soksi za ngozi ni kwa sababu kunamtia mtu uzito kule kuzivua. Kwa hivyo hakuna tofauti kati ya soksi za ngozi ambazo ni nyembamba na soksi za ngozi ambazo ni nene, zilizopasukapasuka na zilizosalimika. Muda wa kuwa bado zinaitwa “soksi za ngozi” basi itafaa kupangusa juu yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/165-166)
  • Imechapishwa: 05/05/2021