10. Dalili ya kwamba washirikina waliopigwa vita na Mtume walikuwa wakiikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah

Ukitaka dalili ya kwamba washirikina hawa ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita walikuwa wanashuhudia hili soma Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka kwa aliyekufa na anayemtoa aliyekufa kutoka aliye uhai na nani anayeendesha mambo yote?” Watasema: “Ni Allaah.” Basi sema: “Je, basi kwa nini hamuwi wenye kumuogopa Yeye?” (Yuunus 10 : 31)

Na kauli Yake:

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

“Sema: “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo ndani yake mkiwa mnajua?” Watasema: “Ni vya Allaah.” Sema: “Je, basi hamfikirii?” Sema: “Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ´Arishi kubwa?” Watesema: “Ni ya Allaah.” Sema: “Je, basi hamwogopi?” Sema: “Nani katika mikono Yake mna ufalme wa kila kitu Naye ndiye Alindae na wala hakuna yeyote awezae kumlinda, ikiwa mnajua?” Watasema: “Ni Allaah.” Sema: “Basi vipi mnazugwa?”” (al-Muuminuun 23 : 84-89)

Kuna Aayah zingine mfano wa hizo

MAELEZO

Maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah):

Ukitaka dalili ya kwamba washirikina hawa ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita walikuwa wanashuhudia hili… “

Bi maana Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na wakati huo huo ni wenye kushirikisha katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Endapo utataka dalili juu ya masuala haya makubwa ambayo kwayo inatambulika haki kutokamana na batili, basi soma maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka kwa aliyekufa na anayemtoa aliyekufa kutoka aliye uhai na nani anayeendesha mambo yote?” Watasema: “Ni Allaah.” Basi sema: “Je, basi kwa nini hamuwi wenye kumuogopa Yeye?” (10:31)

Washirikina walikuwa wakikubali ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Muumbaji, Mruzukaji, Mwenye kuyaendesha mambo ya viumbe Wake. Hakuna yeyote katika wao aliyekuwa akiyapinga haya. Amesema (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini… “

Ni nani aliyeleta riziki hii mnayokula, kunywa, kuvaa na kupanda? Je, imeletwa na masanamu? Masanamu ni vitu visivyokuwa na uhai. Kadhalika mawe, miti, maiti na makaburi vyote hivi havikuleteeni riziki zenu. Kwa hiyo walikuwa ni wenye kukubali kuwa masanamu yao hayaumbi na wala hayaruzuku. Amesema (Ta´ala):

أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ

“… au nani anayemiliki kusikia na kuona… “

Ni nani ambaye kakuumbia vyote hivi? Kuna yeyote asiyekuwa Allaah aliyeviumba? Hivi mmeona kiumbe yeyote anamrudishia mwengine usikizi pale unapomuondoka? Kuna yeyote anaweza kumrudishia mwengine uoni unapomuondoka? Lau watu wa ardhini wote watakusanyika kwa ajili ya kumrudishia machoni mwake uoni basi hawatoweza kufanya hivo. Si masanamu, madaktari wala wasomi bingwa. Washirikina walikuwa wakikubali kwamba masanamu yao hayafanyi chochote katika hayo. Amesema (Ta´ala):

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَخَذَ اللَّـهُ سَمْعَكُمْ وَأَبْصَارَكُمْ وَخَتَمَ عَلَىٰ قُلُوبِكُم مَّنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِهِ

“Sema: “Mnaonaje ikiwa Allaah Atakuondoleeni kusikia kwenu na kuona kwenu na Akapiga mhuri juu ya nyoyo zenu; je, ni muabudiwa wa haki gani ghairi ya Allaah Atakuleteeni hayo?”” (06:46)

Hakuna yeyote awezaye kuyajibu maswali haya na wala hakuna yeyote awezaye kurudisha usikizi na uoni isipokuwa Allaah pekee.

وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ

“… na nani anayemtoa aliye hai kutoka kwa aliyekufa na anayemtoa aliyekufa kutoka aliye uhai… “

Haya ni katika maajabu ambapo Anamtoa hai kutoka kwa aliye maiti, Anaitoa riziki kutoka kwenye mbegu na Anamtoa muumini kutoka kwa kafiri.

وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ

“… na anayemtoa aliyekufa kutoka aliye uhai… “

Anamtoa kafiri kutoka kwa muumini na kifaranga kutoka kwenye yai. Ambaye anaweza kufanya hivo ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ

“…. na nani anayeendesha mambo yote?”

Huu ni ujumla. Kwa msemo mwingine ni kwamba mambo yote kuanzia umauti, uhai, maradhi, afya njema, ukafiri, imani, utajiri, ufakiri, usiku, mchana, nguvu, unyonge na ufalme Anampa hayo yule Amtakaye na Anampokonya hayo yule Amtakaye. Ni nani anayefanya kupitika kwa yale mageuzo na mabadiliko yanayopitika katika ulimwengu huu?

فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ

“Watasema: “Ni Allaah.”

Ndipo Allaah akamwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

Basi sema: “Je, basi kwa nini hamuwi wenye kumuogopa Yeye?””

Midhali mnakubali kuwa mambo haya yako mkononi mwa Allaah na kwamba masanamu yenu hayafanyi kitu katika hayo, ni kwa nini basi msimche Allaah (´Azza wa Jall) na mkampwekesha kwa ´ibaadah? Kwa kuwa msipomcha Allaah basi Allaah atakuadhibuni kwa kuwa amekusimamishieni hoja na ameukata udhuru wenu. Hakuna kilichobaki isipokuwa ni adhabu midhali mmekwishajua haki na hamtaki kuifanyia kazi.

فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ

“Basi Huyo ndiye Allaah Mola wenu wa haki. Kuna nini baada ya haki kama si upotofu? Basi mnageuzwa wapi?” (10:32)

Imekubainikieni kuwa ´ibaadah ni haki ya Allaah (Ta´ala) na kwamba hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah pekee. Hivyo basi, msipomuabudu ni upotevu. Kuna nini tena baada ya haki, ambayo ni Tawhiyd na kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah, isipokuwa ni upotevu, ambao ni shirki.

Kwa hiyo muislamu anatakiwa kutahadhari na aikimbilie haki pale itapombainikia na khaswa katika mambo yanayohusiana na Tawhiyd na ´Aqiydah. Aikimbilie haki pale itapombainikia na aogope kuibanduka na kutoirudi. Amesema (Ta´ala):

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

“Sema: “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo ndani yake mkiwa mnajua?” Watasema: “Ni vya Allaah.” Sema: “Je, basi hamfikirii?” Sema: “Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ´Arishi kubwa?” Watesema: “Ni ya Allaah.” Sema: “Je, basi hamwogopi?” Sema: “Nani katika mikono Yake mna ufalme wa kila kitu Naye ndiye Alindae na wala hakuna yeyote awezae kumlinda, ikiwa mnajua?” Watasema: “Ni Allaah.” Sema: “Basi vipi mnazugwa?””

Aayah hizi zilizokuja katika Suurah “al-Muuminuun” ni kama mfano wa Aayah zilizokuja katika Suurah “Yuunus” ambazo zimetajwa na mwandishi. Ni kama mfano vilevile wa Aayah nyenginezo ambazo zimekariri kuwa washirikina walikuwa wakikubali utendaji kazi wa Allaah lakini hata hivyo wakifanya upinzani katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Amesema (Ta´ala):

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ

“Sema: “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo ndani yake mkiwa mnajua?” Watasema: “Ni vya Allaah.”

Maadamu ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Allaah, ni vipi mnaabudu masanamu yasiyomiliki kitu na mnayaabudu pia makaburi na wale maiti ambao watu wake hawana uhai wowote?

أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

“Je, basi hamfikirii?”

Hivi kweli hamfikirii kuwa Yule anayemiliki ardhi na vilivyomo ndani yake ndiye ambaye anastahiki kuabudiwa pasi na haya masanamu mnayoabudu? Huku ni kusimamisha hoja dhidi yao kwa yale wanayoyakubali juu ya yale wanayoyakanusha. Wao wanakubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na wanakanusha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 18-21
  • Imechapishwa: 08/10/2016