09. Hali ya washirikina wa kiarabu wa hapo kale

Allaah alimtuma kwa watu ambao wanaabudu, wanahiji, wanatoa swadaqah na wanamdhukuru Allaah kwa wingi, lakini waliwafanya baadhi ya viumbe kuwa, waasitwah, wakati kati baina yao na baina ya Allaah (Ta´ala). Wanasema: “Tunataka kutoka kwao kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) na tunataka uombezi wao Kwake; kama mfano wa Malaika, ´Iysa, Maryam na wengineo katika watu wema. Allaah (Ta´ala) akawatumia Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awajadidie dini ya baba yao (´alayhis-Salaam) na kuwaeleza ya kwamba kujikurubisha huku na itikadi hii ni haki ya Allaah peke Yake, haisihi kufanyiwa katika hayo mwengine yeyote asiyekuwa Allaah, si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumwa, tusiseme wasiokuwa hao. Vinginevyo washirikina hawa walikuwa wakishuhudia ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji pekee asiyekuwa na mshirika, na kwamba hakuna anayeruzuku isipokuwa Yeye, na hakuna anayehuisha wala kufisha isipokuwa Yeye, na wala hakuna anayeendesha mambo isipokuwa Yeye na kwamba mbingu zote saba na vilivyomo ndani yake, na ardhi saba na vilivyomo ndani yake, vyote hivyo [walikuwa wakiamini kuwa] ni viumbe Vyake na viko chini ya uendeshaji na Uwezo Wake.

MAELEZO

Washirikina wa kiarabu waliotumiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakimuabudu Allaah lakini hata hivyo haikuwafaa kitu ´ibaadah hii pindi ilipokuwa imechanganyika na shirki kubwa. Hakuna tofauti sawa ikiwa kile anachoshirikishwa nacho Allaah (Subhaanah) ni sanamu, mja mwema, Mtume aliyetumwa au Malaika aliyekaribu au malengo ya yule mshirikina ikawa kile anachokiabudu sio mshirika wa Allaah bali yeye anakichukulia tu kama njia inayomfikisha na kumkurubisha kwa Allaah. Hayo yamefahamisha mambo mawili:

La kwanza: Kukubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah peke yake haitoshi kumwingiza mtu katika Uislamu na wala haisalimishi damu, mali na haimuokoi mtu na adhabu ya Allaah.

La pili: ´Ibaadah ya Allaah ikichanganyika na kitu katika shirki inaiharibu. ´Ibaadah haisihi isipokuwa tu pamoja na Ikhlaasw.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 17
  • Imechapishwa: 08/10/2016