09. Sababu ya nane ya maisha mazuri: Kuondosha sababu za misononeko na kuleta sababu za furaha

8- Miongoni mwa sababu zinazoleta furaha na kuondosha msongo wa mawazo na misononeko ni mtu kujaribu kuziondosha zile sababu zinazoleta misononeko ya roho na pia kujaribu kuleta zile sababu zinazoleta furaha. Hayo yanapitika kwa yeye kusahau yale mambo mabaya yaliyopita ambayo hawezi kuyarudisha na kutambua kwamba kuzishughulisha fikira juu ya mambo hayo ni upuuzi na jambo la muhali na kwamba kitendo hicho ni upumbavu na wendawazimu. Kwa hiyo apambanane na moyo wake kutoyafikiria. Vivyo hivyo apambane na moyo wake na misononeko juu yale yanayokuja huko mbele katika yale mambo anayoyawaza katika umasikini, khofu au mengineyo katika mambo mabaya ambayo anayajengea picha juu ya mustakabali wa maisha yake. Anatakiwa kutambua kuwa yanayokuja huko mbele katika yatayotokea katika mambo ya kheri, shari, mambo ya matumaini na mambo yenye kuumiza na kwamba yako mikononi mwa Mwenye nguvu asiyeshindika, Mwingi wa hekima. Hakuna chochote kilichoko mikononi mwa waja isipokuwa kujaribu tu kufikia zile kheri zake na kujikinga na madhara yake.

Mja anapaswa kutambua kwamba akiziondosha fikira zake kutokamana na ule wasiwasi wa mambo yanayokuja huko mbele, akayaegemeza kwa Mola Wake katika kuyatengeneza na akatulizana juu ya jambo hilo, akiyafanya hayo basi moyo wake utatulizana na hali zake zitatengemaa na ataondokewa na msongo wa mawazo na misononeko.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 15/06/2020