08. Sababu ya saba ya maisha mazuri: Daima kumtazama yule aliye chini yako

7- Miongoni mwa mambo yenye kusaidia sana katika nafasi kama hii ni mtu kutumia yale aliyoelekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh pindi aliposema:

“Mtazameni yule aliye chini kati yenu na wala msimtazame yule aliye juu kati yenu. Kwani kufanya hivo ni haki zaidi msije mkazidharau neema za Allaah juu yenu.”[1]

Hakika mja akiweka mazingatio haya matukufu mbele ya macho yake, basi ataona kuwa amewashinda asilimia kubwa ya viumbe katika afya na vile vinavohusiana nayo, riziki na vile vinavohusiana nayo, pasi na kujali hali itafikia kiasi gani. Kwa hayo misononeko, msongo wa mawazo na uchugu wake utaondoka na wakati huohuo ile furaha yake na kule kutamani neema za Allaah kutazidi ambazo amewashinda wengine wengi ambao wako chini yake.

Kila ambavo mja atazidi kuzingatia neema za Allaah zenye kuonekana na zilizojificha, za kidini na za kidunia, basi ataona kuwa Mola wake amempa kheri nyingi na pia amemwepusha na shari nyingi. Hapana shaka kwamba jambo hili linaondosha masikitiko na misononeko na wakati huohuo kunampelekea kufurahi na kuliwazika.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 15/06/2020