08. Kwenda misikiti ya mbali kwa ajili ya kisomo kizuri cha imamu

Swali: Ni ipi hukumu ya kutafuta misikiti kwa lengo la sauti nzuri ya yule imamu kutokana na unyenyekevu na uhudhuriaji wa moyo unaozalikana kwa jambo hilo?

Jibu: Kinachodhihiri – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwamba hapana neno kufanya hivo ikiwa lengo ni mtu kutaka msaada kupitia jambo hilo wa unyenyekevu katika swalah yake na kunamfanya kupata utulivu na moyo wake kutulia. Kwa sababu sio kila sauti inastarehesha. Ikiwa malengo yake ya kwenda katika sauti ya fulani ni kwa ajili ya kutaka kheri na ukamilifu wa unyenyekevu ndani ya swalah yake hakuna neno kufanya hivo. Bali anaweza kushukuriwa kwa jambo hilo na akalipwa kutegemea nia yake. Mtu anaweza kupata unyenyekevu nyuma ya imamu fulani na asipate unyenyekevu nyuma ya imamu mwengine kutokana na ile tofauti kati ya visomo viwili hivyo na swalah mbili hizo. Ikiwa malengo ya kuuendea kwake msikiti ulioko mbali ni kwa ajili ya kusikiliza kisomo chake kizuri, afaidike na jambo hilo na aingiwe na unyenyekevu ndani ya swalah yake… isiwe kwa ajili tu ya matamanio na kutangatanga. Ni sawa ikiwa ni kwa lengo la kufaidika, kupata elimu na kwa lengo la unyenyekevu ndani ya swalah. Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Watu wenye ujira mkubwa zaidi katika swalah ni wale wenye kutembea kutokea sehemu ya mbali.”[1]

Ikiwa lengo lake jengine ni kwa ajili ya kuongeza zile hatua za miguu basi hayo ni malengo mazuri.

[1] al-Bukhaariy (614) na tamko ni lake na Muslim (1064).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 10/04/2022