09. Kuhamahama kati ya misikiti kwa ajili ya kumtafuta imamu mwenye sauti nzuri

Swali: Ni ipi hukumu ya kuhamahama kati ya misikiti kwa njia ya kwamba kila usiku yuko kwenye msikiti mwingine kwa ajili ya kutafuta sauti nzuri?

Jibu: Sioni ubaya wa jambo hilo ijapokuwa namili zaidi ya kwamba alazimiane na ule msikiti ambao moyo wake unapata utulivu na unyenyekevu zaidi ndani yake. Kwa sababu anaweza kwenda katika msikiti mwingine asipate yale aliyoyapata katika ule msikiti wa kwanza katika unyenyekevu na utulivu. Kwa hivyo mimi naipa nguvu zaidi – kutegemea zile kanuni za ki-Shari´ah – ya kwamba akimpata imamu ambaye anapata utulivu na unyenyekevu zaidi kutokana na kisomo na swalah yake basi alazimiane na jambo hilo au aswali naye kwa wingi. Jambo liko wazi na halina neno na himdi zote ni stahiki ya Allaah. Akihamia kwa imamu mwengine sitambui ubaya wa kufanya hivo ikiwa malengo yake ni kheri na hayana malengo mengine kama vile kujionyesha. Lakini lililo karibu zaidi, kwa mujibu wa zile kanuni za ki-Shari´ah, ni kwamba alazimiane na ule msikiti ambao ndani yake kuna unyenyekevu, utulivu na kisomo kizuri au kuna waswaliji wengi kwa sababu yake pindi anaposwalisha basi waswaliji wanakuwa wengi kwa ajili ya kumfuata au kwa sababu anawapa faida na hawana mwengine wa kuwapa faida na anawakumbusha katika baadhi ya nyakati au anawatolea darsa. Kwa msemo mwingine wanapata faida kwa uwepo wake. Ikiwa mambo ni hivo basi kile kitendo chake cha yeye kufuata msikiti huo ambao ndani yake kuna faida kutoka kwake au kutoka kwa mtu mwengine au moyo wake unakuwa karibu zaidi kuingiwa na unyenyekevu, utulivu na kuhisi ladha ya swalah, basi yote hayo ni mambo yanayotakikana.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 10/04/2022