08. Hapa ndipo haitofaa kwa mwanamke kuonyesha uso na mikono yake

Pengine kutokana na sababu hiyo ndio iliyomfanya Haafidhw Ibn-ul-Qattwaan kuacha kuyashughulikia maoni haya katika kitabu chake kilichotajwa. Aliyataja tu kama moja miongoni mwa maoni yaliyotajwa tofauti na alivyotaja maoni ya wanazuoni na madhehebu mengine, ambayo ameyataja kwa undani na kwa kuyakagua. Simjui aliyefanya kama alivofanya yeye.

Kisha akataja baadhi ya Hadiyth zinazoweza kutumiwa kama hoja juu ya kufaa kwa mwanamke kuonyesha uso na mikono mbele ya wanamme wa kando naye. Licha ya kuwa amepitwa na Hadiyth nyingi zilizotajwa katika kitabu changu hiki. Amezichambua kwa umakini, akapambanua zilizo Swahiyh na zisizo Swahiyh na akazindua ambazo inasihi kuzijengea kama hoja na ambazo hazisihi kuzijengea kama hoja pasi na kuegema upande wowote.

Kisha baada ya hapo akazungumzia Aayah na akaifasiri tafsiri ya ajabu na inayojulisha kuwa ni kiongozi katika tafsiri ya Qur-aan, Fiqh na Hadiyth. Amethibitisha (Rahimahu Allaah) ya kwamba makatazo ni kwa njia isiyofungamana kwa njia nne na akalipambanua hilo kwa kina. Hata hivyo njia ambayo inatuvutia hapa ni ile ya nne. Amesema:

”Haikufungamanishwa kwa njia ya kile chenye kuonekana. Hapa kuna mambo mawili yaliyovuliwa:

1 – Mapambo. Yamefungamanishwa na:

إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“… isipokuwa yale yanayodhihirika… “

Haya inafaa kwake kuyaonyesha kwa kila mtu.

2 – Waangaliaji wanaotazama mapambo hayo. Wamefungamanishwa waume na wengineo waliotajwa baada yao.”[1]

Baada ya kutaja maoni ya Ibn Mas´uud, maoni ya Maswahabah na wengineo waliokuja baada yao, maoni ya madhehebu na Hadiyth zilizoashiriwa punde, akabainisha maoni yake kwa kifupi:

”Hadiyth zilizotajwa ima zinafahamisha kuonyesha yote katika uso na mikono au sehemu yake kwa njia inayotofautiana na vile yanavyodhihiri maandiko. Lakini ili Aayah iweze kueleweka tofauti na yanavyofahamisha maandiko ni lazima kuwepo dalili inayojuzisha jambo hilo. Vinginevyo tafsiri hiyo itakuwa ya kiholela. Kujengea juu ya hilo ni lazima kuyatendea kazi yale maoni yanayomruhusu mwanamke kuonyesha uso na mikono yake. Lakini kinachobaguliwa ni pale ambapo atakusudia kuyaonyesha kwa ajili ya kutaka kuvutia na kuonyesha uzuri wake. Katika hali hiyo itakuwa haramu. Kwa hivyo ataonyesha yale ambayo kikawaida huonekana. Halazimiki kuyafunika tofauti na yale ambayo kidesturi hufunikwa kama vile kifua na tumbo. Viungo hivyo haifai kwake kabisa kuvionyesha na wala hasamehewi kwa kuonekana kwake. Ni lazima kwake kuvifunika katika hali zote. Madhihirisho haya yanaungwa mkono na maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“… na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika… “

Maana ya Aayah ni kwamba haifai kwake kuonyesha mapambo katika maeneo yake kumuonyesha kiumbe yeyote isipokuwa yale ambayo yamezoeleka kuonekana. Yale yanayoonekana pasi na makusudio ya kuvutia na kufitinisha hayana neno.”

[1] an-Nadhwar fiy Ahkaam-in-Nadhwar (2/15 – muswada).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 04/09/2023