Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ بِسْمِ ٱللَّٰهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”[1]

MAELEZO

Wakati mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) alipotoa hukumu ya ulazima wa kujifunza mambo haya, ndipo akaleta dalili yake. Hii ndio dalili ya mambo manne yaliyotajwa na mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) na kwamba ni lazima kwa mtu kujifunza nayo, kuyafanyia kazi, kulingania kwayo na kusubiri juu yake.

Katika Aayah hii Allaah anaapa kwa alasiri ambayo ni wakati kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi[2]. Ni mahali pa kuondoka na kuchuma mazuri na maovu. Kwa msemo mwingine ni mahali pa kufanya matendo. Alasiri ndio kilichoapiwa.

Maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ

“Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara.”

Bi maana aina ya mtu yuko katika khasara ambayo ni maangamivu[3]. Allaah ameapa kwa ajili ya jambo hili. Yeye ni Mkweli hata kama hakuapa. Lakini amefanya hivo kwa ajili ya kusisitiza.

Shaykh as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Viwango na ngazi za khasara zinatofautiana; khasara inaweza kuwa ya moja kwa moja kama hali ya ambaye amekhasirika duniani na Aakhirah, akakosa neema na akastahiki Moto. Khasara yake inaweza kuwa baadhi ya vipengele kuliko vingine. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah amejumlisha khasara kwa kila mtu. Isipokuwa ambaye amejipamba kwa sifa nne.”[4]

Maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“.. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”

Hawa ndio washindi na ambao wamebaguliwa kutokana na khasara:

1 – Wameamini imani ya kweli iliyojengeka juu ya elimu. Hakuna elimu sahihi pasi na elimu. Elimu hii ndio suala la kwanza.

2 – Hili ni suala la pili. Kuifanyia kazi elimu hiyo. Mema ni kutekeleza yale ya wajibu na kujiepusha na yale yaliyoharamishwa.

3 – Hili ni suala la tatu. Kulingania kwa Allaah. Ameisifu kuwa ni kulingania katika haki.   

4 – Hili ni suala la nne. Kufanya subira juu ya yale mambo matatu yaliyotangulia.

Kwa hivyo watu wote wako katika khasara na maangamivu isipokuwa wale wenye kusifika kwa sifa hizi nne; kuamini imani ambayo imejengeka juu ya elimu, matendo, kuusiana kunako haki ambako ni kule kulingania kwa Allaah na kuusiana kufanya subira. Ambaye atakamilisha sifa hizi, akazisimamisha na akanyooka juu yake basi ushindi wake umekamilika. Anakuwa mshindi. Mwenye kuzipoteza inakamilika khasara yake. Na yule anayepungukiwa na kitu katika mambo hayo, basi anapitwa na ushindi na anapata sehemu katika khasara kwa kiwango cha vile alivyopungukiwa katika mambo haya.

[1] 103:01-03

[2] Tazama ”al-Jaamiy´-ul-Ahkaam al-Qur-aan” (20/178) na ”ad-Durar al-Manthuur” (08/622).

[3] Tazama ”Tafsiyr” ya al-Baghawiy (08/255) na ”Tafsiyr” ya Ibn Kathiyr (08/480).

[4] Tazama ”Tafsiyr” ya as-Sa´diy”, uk. 934.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 19-21
  • Imechapishwa: 01/02/2023