07. Ni lazima kufanya subira wakati wa kulingania

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

2 – Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake.”

Bi maana ukishajua, ukafanyia kazi kisha ukawalingania watu katika kumwabudu Allaah pekee, basi tambua kuwa ni lazima ufikwe na maudhui. Kwa sababu ambaye anawalingania watu anasimama mbele yao na anasimama mbele ya matamanio yao. Kwa msemo mwingine anawazuia kuyafanya mambo ambayo wanayapenda. Kwa hivyo wakimuudhi – ima kwa maneno au kwa vitendo – basi anapaswa kusubiri juu ya maudhi yanayompata. Maudhi hayo ima yakawa kwa maneno kwa njia ya kutukanwa au kwa kushambuliwa kwa mkono. Ni lazima usubiri. Usiposubiri basi utasimama njiani. Ni lazima usubiri juu yale yanayokupata katika kutukanwa, matusi, kipigo au kufungwa.

Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) – na wao ndio mfano wa kuigwa – waliudhiwa katika njia hii lakini wakasubiri. Nuuh aliikaa kwa watu wake muda wa 950 wakimuudhi na mara wakimtuhumu wazimu na mara nyingine uchawi. Vivyo hivyo Huud, Swaalih, Muusa, ´Iysaa, Shu´ayb na Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) alifikwa na yakumfika. Alifikia mpaka kuwekewa shingoni mwake matumbo ya mtoto wa ngami (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1] na baadhi ya makafiri wakamkaba koo mpaka akaja Abu Bakr na kumtetea[2]. Walijaribu kumuua mara nyingi.

Kwa hivyo njia ya ulinganizi haikutandikiwa maridi. Ni lazima kufanya subira. Ambaye hafanyi subira husimama njiani. Kwa ajili hiyo Allaah amemwambia Mtume Wake  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ

“Basi subiri kama walivyosubiri wenye azimio madhubuti katika Mitume.”[3]

Kwa kumalizia; haya ndio mambo manne ambayo ni lazima kwa muislamu kujifunza nayo:

1 – Elimu.

2 – Kuifanyia kazi.

3 – Kuilingania.

4 – Kusubiri juu ya maudhi ndani yake.

[1] Muslim (1794).

[2] al-Bukhaariy (3678).

[3] 46:35

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 19
  • Imechapishwa: 01/02/2023