Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Matendo yatakuja siku ya Qiyaamah. Swalah itakuja na iseme: “Ee Mola! Mimi ndio swalah.” Aseme: “Uko katika kheri.” Kisha ije swadaqah na iseme: “Ee Mola! Mimi ndio swadaqah.” Aseme: “Uko katika kheri.” Kisha ije swawm na isema: “Ee Mola! Mimi ndio swawm.” Aseme: “Uko katika kheri.” Halafu yaje matendo mengine yote na aseme: “Uko katika kheri.” Halafu kuje Uislamu na usema: “Ee Mola! Wewe ni as-Salaam na mimi ndio Uislamu.” Aseme: “Uko katika kheri.” Leo hii nitachukua na kupeana kutokana na wewe.” Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kutoka kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

Ameipokea Ahmad.

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume wa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kufanya tendo lisiloafikiana na amri yetu litarudishwa.”

MAELEZO

Hii ina maana ya kwamba ni lazima kwa viumbe wote kufata Uislamu na kwamba hakuna kuokoka wala kufaulu kwa viumbe isipokuwa kwa Uislamu. Kama atavosema Allaah:

“Leo hii nitachukua na kupeana kutokana na wewe.”

Yule mwenye kufa juu ya Uislamu ataingia Peponi ima pale mwanzoni tu, ikiwa atasalimika kutokamana na maasi, au baada ya adhabu ambayo Allaah atamkadiria kwa sababu ya maasi aliyokufa juu yake ikiwa Allaah hatomsamehe pale mwanzoni tu. Hakuna uokozi isipokuwa kwa Uislamu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kutoka kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”

Yule mwenye kufa katika dini isiyokuwa Uislamu, haijalishi kitu hata kama atakuwa na mema mengi mfano wa mlima, ni yenye kuharibika:

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا

”Tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, Tutayafanya kuwa ni vumbi lililotawanyika.” (25:23)

Ni lazima kupatikana jambo la kumwabudu Allaah peke yake na mtu ashuhudie ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na kuingia ndani ya Uislamu kwa moyo wake kisha baada ya hapo mtu aufuatishie matendo. Yule ambaye atanyooka juu ya matendo basi ataingia Peponi pale mwanzoni. Na yule mwenye kufanya mapungufu kwenye chochote katika matendo ambayo yanampasa au akafanya baadhi ya maasi ambayo Allaah amemuharamishia, basi ataingia chini ya utashi wa Allaah; Allaah akitaka kumsamehe, atamsamehe, na akitaka kumuadhibu, atamuadhibu kwa kiwango cha madhambi alionayo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakaye.” (04:48)

Ambaye ataongozwa na Allaah katika Uislamu na akasalimika kutokamana na shirki, basi yuko katika njia ya uokozi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 13/10/2020