Swali: Leo kunazungumziwa sana uelewa wa mambo ya kisasa (فقه الواقع), baadhi wanachupa mipaka na wengine wanazembea. Je, kuna kigezo kilichowekwa katika Shari´ah juu ya jambo hilo? Je, ipo dalili yoyote kwamba Salaf walikuwa na uelewa kama huo?

Jibu: Uelewa wa mambo ya kisasa maana yake ni kuwa na uelewa wa hali za watu wanazoishi. Hali za watu zinatakiwa kujilikana kwa mtu ili apate kujua yale wanayoishi ndani yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliashiria maana hii wakati alipomtuma Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) kwenda Yemen na akasema:

”Hakika wewe unawaendea watu wa Kitabu.”

Hivyo akamweleza kuhusu hali yao. Lakini uelewa huu haijuzu kabisa ukakiuka uelewa wa dini. Jengine ni kwamba uelewa huu hautakiwi kuwafanya vijana na wengine kujali matukio ambayo hawawezi kuyarekebisha, endapo kama kweli watataka kuyarekebisha. Uelewa katika dini ndio msingi.  Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa ufahamu katika dini.”[1]

Tunahitajia uelewa wa mambo ya kisasa ili kuweza kutekeleza hukumu ya dini kwa watu. Kwa sababu huwezi kuhukumu kama swalah ya mtu imeharibika mpaka kwanza uwe na utambuzi kama kweli imeharibika, au kwamba funga yake imeharibika mpaka kwanza uwe na utambuzi kama kweli imeharibika. Lakini kama tulivyotangulia kusema haijuzu kabisa uelewa huu wa mambo ya kisasa ukakiuka uelewa katika dini kwa njia ya kwamba mtu akawa hana hamu nyingine isipokuwa tu kusoma magazeti, majarida na mengineyo na akaipa mgongo Qur-aan na Sunnah.

[1] al-Bukhaariy (71).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (11 B)
  • Imechapishwa: 13/10/2020