Imaam, Fiqiyh wa dini, mwanachuoni wa ´Iraaq; Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit bin Zuutwaa at-Taymiy, al-Kuufiy, mtumwa aliyeachwa huru na Taymullaah bin Tha´labah. Inasemekana kuwa anayo asili ya kipersia.

Alizaliwa mwaka wa 80 katika uhai wa Maswahabah wadogowadogo. Alimuona Anas bin Maalik wakati alipowajia Kuufah. Lakini hata hivyo haikuthibiti kusikia Hadiyth hata moja kutoka kwa yeyote katika wao.

Amepokea kutoka kwa ´Atwaa´ bin Abiy Rabaah na ndiye mwalimu wake mkubwa na mbora wao kutokana na aliyoyasema mwenyewe, kutoka kwa ash-Sha´biy, Twaawuus, lakini haikusihi, ´Amr bin Diynaar, Naafiy´, mtumwa aliyeachwa huru na Ibn ´Umar, az-Zuhriy, Abu Ishaaq ash-Shabiy´iy na wengineo.

Waliopokea kutoka kwake ni mtoto wake Hammaad bin Abiy Haniyfah, ´Abdullaah bin al-Mubaarak, Zufar, ´Abdur-Razzaaq, Abu Nu´aym, Muhammad bin al-Hasan ash-Shaybaaniy, Wakiy´, Abu Hamzah as-Sukkariy, Abu Yuusuf Ya´quub al-Answaariy na wengineo.

Ahmad al-´Ijliy amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa ni muuzaji hariri.”

´Abdur-Rahmaan al-Muqriy amesema:

“Abu Haniyfah ni katika watu wa Babeli.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa mwaminifu. Alikuwa hasimulii Hadiyth isipokuwa ameihifadhi na wala hasimulii kile ambacho hakuhifadhi.”

Abu Haniyfah alisema kumwambia mwalimu wake Hammaad bin Abiy Sulaymaan:

“Nilifika Baswrah nikafikiri kuwa sintoulizwa chochote isipokuwa nitakijibu. Wakaniuliza mambo ambayo sikuwa na majibu yake. Nikaiambia nafsi yangu kwamba sintotengana na Hammaad mpaka atakapofariki. Nikatangamana naye kwa miaka kumi na nane.”

´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Lau Allaah asingenisaidia kwa Abu Haniyfah na Sufyaan, basi ningekuwa kama watu wengine.”

Hujr bin ´Abdil-Jabbaar ameeleza kwamba kulisemwa kuambiwa al-Qaasim bin Ma´n:

“Je, unataka kuwa katika wanafunzi wa Abu Haniyfah?” Akasema: “Watu hawakupatapo kukaa na mtu mwenye manufaa kama kukaa na Abu Haniyfah.” Njoo tumwendee.” Walipomfikia, wakalazimiana naye na wakasema: “Sijawahi kuona mtu kama huyu.”

Asad bin ´Amr amesema:

“Abu Haniyfah aliswali ´Ishaa na Fajr kwa wudhuu´ wa miaka arobaini.”

Abu Yuusuf amesema:

“Kipindi nilipokuwa natembea na Abu Haniyfah nilimsikia bwana mmoja akisema: “Huyu ndiye Abu Haniyfah. Halali usiku.” Ndipo Abu Haniyfah akasema: “Naapa kwa Allaah hakusimuliwi juu yangu kwa kitu nisichokifanya.” Alikuwa akikesha usiku kuswali, kunyenyekea na kuomba du´aa.”

´Abdur-Rahmaan bin Muhammad bin al-Mughiyrah amesema:

“Nilimuona Abu Haniyfah akiwa mtumzima akiwapa watu fatwa kwenye msikiti wa Kuufah. Juu ya kichwa chake alikuwa na kofia nyeusi na ndevu.”

Abu Yuusuf amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa ni mtu wa kati na kati. Alikuwa na umbile zuri na mwenye ufaswaha wa kuzungumza.”

Hammaad bin Abiy Haniyfah amesema:

“Baba yangu alikuwa mrembo. Alikuwa kahawia na muonekano mzuri. Alikuwa ni mwenye kujitia manukato kwa wingi na mzuri. Hazungumzi isipokuwa pindi anapojibu swali na wala hayaingilii mambo yasiyomuhusu.”

´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Sijamuona mtu mtulivu zaidi katika vikao vyake kama Abu Haniyfah. Wala mtu ambaye ana mwenendo mzuri na ulaini kama Abu Haniyfah.”

Qays bin Rabiy´ amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa mwenye kujichunga na mchaji Allaah.”

Shariyk amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa mwenye maneno machache na mwenye akili sana.”

Abu ´Aaswim an-Nabiyl amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa akiitwa “kigingi” kwa sababu ya kuswali kwake sana.”

Abu Yuusuf amesema:

“Abu Haniyfah alikuwa akisoma Qur-aan nzima kila usiku kwenye Rak´ah.”

Yaziyd bin Haaruun amesema:

“Sijaona mtu ambaye ni mpole sana kama Abu Haniyfah.”

Abu Mu´aawiyah ad-Dhaariyr amesema:

“Ni katika Sunnah kumpenda Abu Haniyfah.”

al-Khuraybiy amesema:

“Hakuna anayemsema vibaya Abu Haniyfah isipokuwa hasidi au mjinga.”

´Aliy bin ´Aaswim amesema:

“Lau ingelipimwa elimu ya Abu Haniyfah na elimu ya watu waliokuwa katika zama zake, basi elimu yake ingelikuwa na uzito zaidi.”

Hafsw bin Ghayyaath amesema:

“Maneno ya Abu Haniyfah katika Fiqh ni yenye kudhibiti zaidi kuliko mshairi – hakuna anayemtia kasoro isipokuwa tu mjinga.”

Inasemekana kwamba al-A´mash aliulizwa maswali fulani akajibu:

“Hakuna anayeyajua haya isipokuwa mfanyabiashara ya hariri an-Nu´maan bin Thaabit. Naona kuwa amebarikiwa katika elimu yake.”

Hariyr amesema:

“Mughiyrah alinambia: “Keti na Abu Haniyfah. Lau Ibraahiym an-Nakha´iy angelikuwa hai basi angeliketi naye.”

´Abdullaah bin al-Mubaarak amesema:

“Abu Haniyfah ndiye bingwa zaidi wa watu katika Fiqh.”

Wasifu wake unaweza kujazwa kwa mijeledi mingi – Allaah amrehemu. Alikufa shahidi mwaka 150 gerezani. Alikuwa na miaka sabini na kaburi lake liko Baghdaad – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (6/390)
  • Imechapishwa: 13/10/2020