08. Lazima kwa viumbe wote kumfuata Muhammad

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

“Na Tumekuteremshia Kitabu hali ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu.” (16:89)

an-Nasaa´iy na wengine wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona mikononi mwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) karatasi ya Tawraat akasema:

“Ee mwana wa al-Khattwaab! Una shaka? Nimekufikishieni waziwazi kabisa. Lau Muusa angelikuwa hai hii leo mkamfuata badala ya kunifuata mimi basi mgelikuwa mmepotea.” Ndipo ´Umar akasema: “Nimeridhia Allaah kuwa Mola Wangu, Uislamu kuwa dini yangu na Muhammad kuwa Mtume wangu.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Lau Muusa angelikuwa hai hii leo asingelikuwa na namna isipokuwa kunifuata.”

MAELEZO

Haya yako wazi katika maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kutoka kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.” (24:63)

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.” (59:07)

Ni lazima kwa watu wote kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lau Muusa, ´Iysaa na wengineo wangelikuwa hai basi wasingelikuwa na namna nyingine isipokuwa kumfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye katumilizwa kwa watu wote:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعاً

“Sema: “Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.” (07:158)

Ni lazima kwa viumbe wote, kuanzia mwanamme na mwanamke, mwarabu na asiyekuwa mwarabu, majini na watu, kumfuata yeye  na kunyenyekea Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa vile ilivyokuja katika Qur-aan Tukufu na Sunnah Takatifu. Haifai kwao kutoka nje ya hayo.

[1] Ahmad (3/387), ad-Daarimiy (436), Abu Ya´laa (4/102) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 13/10/2020