09. Makatazo ya kujinasibisha na jina zaidi ya Uislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِي هَـٰذَا

“Yeye Ndiye hapo kabla [katika Vitabu vya awali] na katika [Kitabu] hiki aliyekuiteni “waislamu”.” (22:78)

al-Haarith al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakuamrisheni mambo matano ambayo Allaah ameniamrisha kwayo; usikivu, utiifu, Jihaad, Hijrah na mkusanyiko. Hakika yule mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri basi amevua kamba ya Uislamu kutoka shingoni mwake isipokuwa ikiwa kama atajirudi. Mwenye kuita wito wa kipindi cha kikafiri ataadhibiwa Motoni.” Mtu mmoja akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hata kama ataswali na kufunga?” Akajibu: “Hata kama ataswali na kufunga. Enyi waja wa Allaah! Iteni kwa wito wa Allaah; Yeye ndiye kakwiteni “waislamu” na “waumini”.”[1]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye amesema:

“Hadiyth ni Hasan na Swahiyh.”

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri na akafa, amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pia:

“Mnaita wito wa kipindi cha kikafiri ilihali niko kati yenu?”

MAELEZO

Haya ni matahadharisho juu ya wito wa kipindi cha kikafiri. Kama mfano wa ´ee watu wa fulani´. Haitakikani. Inatakiwa kusema ´ee watu wa Tawhiyd`, ´ee watu wa imani`. Waislamu wote ni ndugu. Wanapojiwa na vita haifai kujinasibisha na kuitana ´ee fulani`, ´ee Qahtwaaniy` na´ee kizazi cha mtu fulani`. Wao ni kitu kimoja. Waislamu ni kitu kimoja. Mtu asiite wito wa kipindi cha kikafiri. Kwa ajili hii wakati Muhaajiruun waliposema:

”Enyi Muhaajiruun.”

Answaar wakasema:

”Enyi Answaar.”

Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mnaita wito wa kipindi cha kikafiri ilihali niko kati yenu?”

Kilicho wajibu kwa watu ni kuitana kwa jina la Uislamu. Kwa mfano wa ´enyi ndugu`, ´enyi waislamu` na ´enyi waumini`. Vivyo hivyo wakati wa kuombana msaada na kuhimizana. Watu wahamasishwe vita kwa kutumia jina la Uislamu na imani.

[1] Ahmad (4/130), at-Tirmidhiy (2863), Ibn Hibbaan (14/125), Ibn Khuzaymah (3/195) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 13/10/2020