Swali: Tunakuomba muheshimiwa kwa mnasaba wa usiku wa Qadar kuwazungumzia waislamu wote kwa jumla juu ya mnasaba huu mtukufu.

Jibu: Usiku wa Qadar ndio usiku bora kabisa. Ndani yake Allaah ameteremsha Qur-aan. Ameeleza (Subhaanah) ya kwamba ni usiku ulio bora kuliko miezi elfu moja na umebarikiwa na kwamba ndani yake kunabainishwa kila jambo la hekima. Allaah (Subhaanah) amesema mwanzoni mwa Suurah “ad-Dukhaan”:

حم وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Haa Miym. Napaa kwa Kitabu kinachobainisha! Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa – hakika Sisi tumekuwa [daima ni] wenye kuonya [watu] – Humo [katika usiku huo] hupambanuliwa kila jambo la hikmah na jambo [Tunalokadiria ni lenye] kutoka Kwetu – hakika Sisi [daima] ndio wenye kutuma [wajumbe Wetu kwa mafunzo na mwongozo]. – Ni Rahmah kutoka kwa Mola wako, hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[1]

Allaah (Subhaanah) amesema:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi Tumeiteremsha katika usiku wa Qadar. Na nini kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadar? Usiku wa cheo ni mbora kuliko miezi elfu; wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa [ajili ya kutekeleza] kila jambo [Lake]. [Usiku huo kunakuwa na] amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[2]

Imesihi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesimama usiku wa Qadar kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[3]

Kusimama kunajumuishwa swalah, Adhkaar, du´aa, kusoma Qur-aan na matendo mengine ya kheri. Suurah hii imefahamisha kuwa matendo mema ndani yake ni bora kuliko matendo ya miezi elfu moja. Hii ni fadhila kubwa na rehema za Allaah kwa waja Wake.

Inampasa kila muislamu kuuadhimisha na kuutumia kwa ´ibaadah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa unakuwa katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan na kwamba uwezekano mkubwa ni kuutafuta katika yale masiku ya witiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan na utafuteni katika kila usiku wa witiri.”[4]

Hadiyth hizi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinafahamisha ya kwamba usiku huu unaweza kupatikana usiku wowote katika yale masiku kumi ya mwisho. Usiku wa Qadar haupatikani kila mwaka usiku mmoja. Unaweza kupatikana tarehe 21, 23, 25, 27 au 29. Unaweza vilevile kupatikana katika masiku ya kawaida.

Atayesimama zile nyusiku zote kumi kwa imani na kwa matarajio haina shaka kuwa atakutana na usiku huu na amefuzu kwa kile alichoahidi Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi zaidi katika masiku haya. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi zaidi katika yale masiku kumi ya mwisho kuliko anavyojitahidi masiku mengine.”[5]

Amesema vilevile:

“Yalipokuwa yakiingia yale masiku kumi anaamka usiku na kuamsha vilevile familia yake, akifanya bidii na akifunga vizuri kikoi chake.”[6]

Mara alikuwa akiyatumia masiku kumi haya akifanya I´tikaaf. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah.”[7]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme nini iwapo atakutana na usiku wa Qadar. Akasema:

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عُفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

“Sema: “Allaah! Hakika Wewe ni msamehevu unayependa kusamehe. Nisamehe.””

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Salaf waliokuja baada yao walikuwa wakijitahidi katika masiku kumi haya ya mwisho na wakijibidisha kwa matendo mema.

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa waislamu wote kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake watukufu (Radhiya Allaahu ´anhum) na Salaf wa Ummah huu. Kwa hiyo wanatakiwa kuyatumia masiku haya kwa kuswali, kusoma Qur-aan na kuomba du´aa na kufanya aina mbalimbali za ´ibaadah kwa imani na kwa kutarajia malipo ili madhambi yao yasamehewe na waokolewe kutokamana na Moto. Ni fadhila, tunuku na ukarimu kutoka Kwake (Subhaanah). Qur-aan na Sunnah vimefahamisha kuwa ahadi hii kuu ni uhalisia endapo kutaepukwa madhambi makubwa. Allaah (Subhaanah) amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Mkijiepusha madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.”[8]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah tano, Ijumaa mpaka Ijumaa na Ramadhaan mpaka Ramadhaan vinafuta vilivyo kati yavyo endapo kutaepukwa madhambi makubwa.”[9]

Ameipokea Imaam Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Miongoni mwa mambo ambayo napasa kuyazindua ni kuwa baadhi ya waislamu utawaona wanajitahidi ndani ya Ramadhaan na wanatubia kwa Allaah kutokana na madhambi ya kale waliyoyafanya, kisha baada tu ya kumalizika Ramadhaan wanarudi katika matendo yao maovu, jambo ambalo lina khatari kubwa. Ni lazima kwa muislamu kutahadhari na jambo hilo na aazimie maazimio ya kweli kuendelea kumtii Allaah na kuacha maasi. Allaah amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“… na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.”[10]

Amesema (Ta´ala) tena:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ 

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah ukweli wa kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.”[11]

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ

”Sisi ni wapenzi wenu katika uhai wa dunia na Aakhirah na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu na mtapata humo yale mtakayoomba – ni takrima kutoka kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.””[12]

Maana ya Aayah ni kwamba wale waliotambua kuwa Allaah ndiye Mola wao, wakamwamini, wakamtakasia ´ibaadah, wakaendelea kuwa na msimamo juu ya hayo, basi Malaika huwapa bishara njema wakati wa kufa ya kwamba wasiwe na khofu na wasihuzunike, na kwamba mafikio yao ni Peponi kwa ajili ya kumwamini kwao Yeye (Subhaanah), kunyooka kwao juu ya kumtii, kuepuka maasi na kumtakasia ´ibaadah Yeye (Subhaanah). Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hiyo ambazo zote zinafahamisha juu ya ulazima wa kuwa na thabiti juu ya haki, kuwa na msimamo juu yake na kutahadhari kuendelea kumuasi Allaah. Miongoni mwa hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ

“Kimbilieni msamaha kutoka kwa Mola wenu na Pepo upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye kumcha Allaah. Ambao wanatoa katika hali ya wasaa na katika hali ya dhiki na wanajizuia ghadhabu na wenye kuwasamehe watu. Na Allaah anapenda wafanyao wema. Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao, basi humtaja Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao – na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah? Na wasiendelee katika waliyoyafanya ilihali wao wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kutoka kwa Mola wao na mabustani yapitayo chini yake mito hali ya kuwa ni wenye kudumu humo – na uzuri ulioje ujira wa watendaji!”[13]

Tunamuomba Allaah atuwafikishe sisi na waislamu wote katika nyusiku hizi na nyenginezo katika yale anayoyapenda na kuyaridhia, atuepushe sote kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Kwani hakika Yeye ni mwingi wa kutoa, Mkarimu.

[1] 44:01-06

[2] 97:01-05

[3] al-Bukhaariy (1901) na Muslim (760).

[4] al-Bukhaariy (2021) na Muslim (1165).

[5] Muslim (1175).

[6] al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174).

[7] 33:21

[8] 04:31

[9] Muslim (2339).

[10] 15:99

[11] 03:102

[12] 41:31-32

[13] 03:133-136

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min A´maal Ramadhwaan, uk. 15-19
  • Imechapishwa: 04/04/2023