Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukishajua kuwa Allaah amekuumba ili umwabudu Yeye, basi jua ya kwamba ´ibaadah haiitwi kuwa ni ´ibaadah, pasi na Tawhiyd. Kama jinsi kuswali hakuitwi kuswali, pasi na wudhuu´. Shirki ikichanganyika na ´ibaadah inabatilika kama jinsi wudhuu´ unavyobatilika unapoingiliwa na hadathi.

MAELEZO

Tawhiyd ni kumtakasia Allaah (Ta´ala) ´ibaadah na kumpwekesha kwa ´ibaadah. Mtu asitumbukie ndani ya shirki. Akiingia ndani ya shirki Tawhiyd inaondoka na Tawhiyd ikiondoka basi ´ibaadah inaharibika na kubatilika. ´Ibaadah sahihi haiwi isipokuwa pamoja na Tawhiyd.

´Ibaadah haiitwi ´ibaadah isipokuwa pamoja na kumtakasia nia Allaah. Kwa maana nyingine ´ibaadah haiwi isipokuwa kwa kukufuru Twaaghuut. Nako ni kule kujitenga mbali na kila kinachoabudiwa badala ya Allaah. Mtu ajitenge navyo, avikanushe, avichukie, avikemee na awajengee uadui wenye nao.

Mtu akiswali kwa ajili ya Allaah hazingatiwi kuwa amemwabudu Allaah isipokuwa pale atapomtakasia ´ibaadah Allaah. Anaweza kumswalia Allaah na akamswalia mwengine. Kwa ajili hii washirikina walimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Waabudu waungu wetu mwaka mmoja na sisi tumwabudu Mungu Wako mwaka mmoja.”

Ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَوَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُوَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ  وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ  لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ

”Sema: “Enyi makafiri! Siabudu yale mnayoyaabudu.” Na wala nyinyi si wenye kuabudu Yule ninayemwabudu. Na mimi si mwenye kuabudu yale mnayoabudu. Na wala nyinyi si wenye kuabudu Yule ninayemwabudu – nyinyi mna dini yenu nami nina dini yangu.”[1]

Kama ambavyo swalah haiitwi kuwa ni swalah isipokuwa pamoja na twahara. Mtu asipotawadha hazingatiwi kuwa ameswali. Ni kama ambavyo hadathi ikichanganyika na twahara haizingatiwi kuwa ni twahara. Vivyo hivyo shirki ikichanganyika na ´ibaadah basi inaiharibu. Ukishajua kuwa ´ibaadah inapoingiliwa na shirki basi inaiharibu na mwenye nayo anakuwa katika watu wa Motoni, basi hapo ndipo itakupasa kupambanua Tawhiyd na shirki, ´ibaadah sahihi na ´ibaadah iliyoharibika.

Mtu anapomwabudu Mola Wake kisha akafanya shirki basi ´ibaadah yake inaharibika na kubatilika. Aidha ni miongoni mwa washirikina na waabudia masanamu. Tunamuomba Allaah usalama na afya. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَن يَعْمُرُواْ مَسَاجِدَ الله شَاهِدِينَ عَلَى أَنفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ

“Si haki kwa washirikina kuamirisha misikiti ya Allaah hali ya kuwa wanajishuhudia nafsi zao kwa ukafiri.”

Bi maana matendo yao yanatosha kuwa ni ushahidi dhidi yao:

أُوْلَئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ

”Hao yamebatilika matendo yao na katika Moto wao ni wenye kudumu.”[2]

[1] 109:01-06

[2] 09:17

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 04/03/2023