06. Mitume wametumwa na kukateremshwa vitabu kwa lengo hili

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuogoze katika kumtii – ya kwamba Haniyfiyyah ni dini ya Ibraahiym, nayo ni kumwabudu Allaah peke yake hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia Yeye dini. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”[1]

MAELEZO

Husemwa dini na kukakusudiwa ´ibaadah, malipo na hesabu. Allaah (Ta´ala) amemwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufuata Haniyfiyyah. Amesema (Ta´ala):

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

 “Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani ya Ibraahim iliyo safi na kutakasika na hakuwa miongoni mwa washirikina.”[2]

Maana yake ni hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Haniyfiyyah ndio Tawhiyd. Ni kule kumwabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye nia. Hii ndio maana ya hapana mungu isipokuwa Allaah. Maana yake ni kuwa hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah.

Neno la Tawhiyd ni kumwabudu Allaah pekee sambamba na kuacha shirki, jambo ambalo haliwi isipokuwa kwa kukanusha na kuthibitisha. ´Hapana mungu` ni kukanusha ´isipokuwa Allaah` ni kuthibitisha.

Kuthibitisha ni kule kumwabudu Allaah (Ta´ala). Kukanusha ni kujitenga mbali na kila chenye kuabudiwa badala ya Allaah. Huku ndio kumtakasia nia Allaah.

Kumtakasia nia Allaah kunapatikana kwa kukufuru Twaaghuut na kumwamini Allaah. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[3]

Haniyfiyyah imeitwa hivyo kutokana na neno haniyf, ambako ni kule kujiengua. Mtu anajiengua kutokana na shirki. Inaitwa pia Uislamu na mila ya ukafiri kwa sababu imejiengua kutokana na ukafiri na ni yenye kunyooka kwa dhati yake. Kwa msemo mwingine ni kwamba unatakiwa kumlenga Allaah kwa ´ibaadah hizi na uzikanushe kutoka kwa wengine. Umwabudu Allaah kwa kumuomba Yeye na usimwombe mwengine, umwabudu Allaah kwa kumchinjia Yeye na usimchinjie mwengine, umwabudu Allaah kwa kumsujudia Yeye na usimsujudie mwengine. Ni lazima kumwabudu Allaah Mmoja pamoja na kumtakasia nia.

Allaah amewaamrisha waja wote kumwabudu Yeye na amewaumba watu na majini kwa ajili ya lengo hilo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[4]

Mitume walitumilizwa na kukateremshwa vitabu kwa ajili ya lengo hili. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[5]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[6]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”[7]

[1] 51:56

[2] 16:123

[3] 02:256

[4] 51:56

[5] 21:25

[6] 17:36

[7] 04:36

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 122-123
  • Imechapishwa: 04/03/2023