07. Hapa ndipo utazingatiwa unamwabudu Allaah pekee

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (RahimahuAllaah) amesema:

“Mja hawi mwenye kuhakiki:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe Pekee tunakuabudu.”[1]

isipokuwa mpaka kwa misingi miwili mitukufu:

1 – Ni lazima kumfuata Mtume (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam).

2 – Ni lazima kumwabudu Allaah kwa kumtakasia nia. Hivi ndivo inahakikiwa Aayah:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe Pekee tunakuabudu…”

Aidha watu inapokuja katika misingi hii miwili wamegawanyika sampuli nne:

1 – Wale wanaomwabudu Allaah kwa kumtakasia nia na kumfuata Mtume (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam). Hao ndio wale wanaohakikisha kikweli Aayah isemayo:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe Pekee tunakuabudu…”

Matendo yao, maneno yao, kutoa kwao, kuzuia kwao, kupenda kwao na kuchukia kwao kote ni kwa ajili ya Allaah. Matangamano yao yote, kwa ndani na kwa nje, ni kwa ajili ya kutafuta uso wa Allaah pekee. Vilevile matendo yao yote na ´ibaadah zao ni zenye kuafikiana na amri ya Allaah na yale Anayoyapenda na kuyaridhia. Haya ndio matendo ambayo Allaah hayakubali kutoka kwa mtendaji isipokuwa yenyewe, na kwayo ndio ambayo ameumba kifo na uhai kwa ajili ya kuwajaribu waja Wake. Kwa hiyo Allaah hayakubali matendo isipokuwa yale yaliyofanywa kwa ajili Yake pekee na kwa mujibu wa amri Yake. Matendo mengine yote ni yenye kurudishwa kwa mwenye nayo na yasiyokuwa na faida yoyote. Kila kitendo ambacho hakina kumwigiliza Mtume (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam) hakimzidishii mwenye nacho isipokuwa kuwa mbali zaidi, kwani Allaah anaabudiwa kutokana na amri Yake na si kwa maono na matamanio.

2 – Wale wanaomwabudu Allaah pasi na kumtakasia Yeye nia wala kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matendo yao hayaafikiani na Shari´ah na wala hayakufanywa kwa ajili ya Allaah pekee. Matendo yao yamefanana na matendo ya wale wenye kujionyesha kwa watu wafanyao matendo ambayo hayakuwekwa katika Shari´ah na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hao ndio viumbe waovu kabisa na wenye kuchukiza zaidi mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Aina hii ya watu mara nyingi hupatikana kwa wale watu waliopotea miongoni mwa wale wenye kujinasibisha na elimu, umasikini na ´ibaadah. Wanafanyia  kazi Bid´ah na upotofu, hujionyesha kwa watu na wanapenda kusifiwa. Wanachotaka ni kusifiwa kwa mambo ambayo hawakuyafanya ambayo ni kufuata, kumtakasia nia Allaah na elimu ambayo hawana. Watu kama hawa wameghadhibikiwa na wamepotea.

3 – Wanamwabudu Allaah kwa kumtakasia nia lakini pasi na kumfuata Mtume (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam). Hivondivowalivo wale wafanya ´ibaadah kwa ujinga ambao wanajinasibisha na kuipa kisogo dunia na umasikini, wanaomwabudu Allaah kwa kusikiliza kelele na upigaji makofi na wale wengine wote wanaomwabudu Allaah kwa isiyokuwa amri Yake na wakaona kuwa ´ibaadah zao zinawakurubisha kwa Allaah.

4 –Wale wanaomfuata Mtume (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam) lakini pasi na kumtakasia nia Allaah. Hivondivowanavofanya wale wenye kujionyesha na wale ambao wanapigana kwa ajili ya kujionyesha na kwa ushabiki na ushujaa, wanahiji ili wasemwe na wanasoma Qur-aan ili wasemwe. Hawa matendo yao kwa uinje ni mema, lakini kimsingi sio mema, na hivyo hayakubaliwi.”[2]

[1]1:5

[2]Madaarij-us-Saalikîn (01/83-85) kwa fafanuzi fulani.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 02/05/2023