07. Hadiyth “Mabwana hawa wawili wanaadhibiwa ndani ya makaburi yao adhabu kali… “

163 – Abu Hurayrah amesema:

“Siku moja tulikuwa tukitembea pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukayapitia makaburi mawili. Akasimama na sisi tukasimama. Rangi ya uso wake ikabadilika mpaka ikajikunja mikono ya kanzu yake. Tukasema: “Ni nini, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kwani hamsikii kile ninachosikia?” Tukasema: “Ni kipi, ee Nabii wa Allaah?” Akasema: “Mabwana hawa wawili wanaadhibiwa ndani ya makaburi yao adhabu kali kwa kitu chepesi.” Tukauliza sababu ambapo akasema: “Mmoja wao alikuwa hajikingi na mkojo na huyo mwingine alikuwa akiwaudhi watu kwa ulimi wake na akieneza umbea kati yao.” Akaitisha makuti mawili ya mtende na akaweka moja katika kila kaburi.” Tukasema: “Je, hayawafaa?” Akasema: “Ndio. Itafanywa nyepesi adhabu yao muda wa kuwa bado ni kijani.”[1]

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake.

Maneno yake kwamba dhambi ilikuwa nyepesi maana yake ni kwamba walikuwa wakidhani kuwa ni nyepesi au kwamba ilikuwa vyepesi kuiepuka, na si kuwa ukweli wa mambo yenyewe kama yenyewe ilikuwa nyepesi. Kwa sababu uvumi ni kitu kilichoharamishwa kwa maafikiano.

[1] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/178-179)
  • Imechapishwa: 05/04/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy